Jadili kwa
mapana Athari katika fasihi linganishi kisha kwa kutumia msingi huo,
onyesha namna athari inavyojitokeza katika; Alfu Lela Ulela:Kitabu cha 1(Kisa
cha walii Wa 11 na mbwa wawili weusi.
Fasihi
linganishi
Dhana
ya Fasihi linganishi kwa kumrejelea Henry Remak (1971) anafasili fasihi
linganishi kama uwanja wa kifasihi unaohusika na uchunguzi na mahusianao ya
kifasihi nje ya mipaka ya nchi moja, pia kati ya fasihi na fani nyinginezo. Kwa
maelezo haya ya Remak tunachoweza kusema ni kwamba fasihi linganishi haiishii
kuangalia mahusino ya kifasihi peke yake bali huangalia mahusiano kati ya
fasihi na fani nyinginezo zisizo za kifasihi.
Athari katia fasihi linganushi.
Fasihi
linganishi imejengeka kwenye msingi kwamba fasihi zozote zinazopatikana katika
ujirani mmoja hazina budi kuathiriana. Kazi za Muyaka Bin Haji zimeathiri kazi
za washairi wa baadaye kama Juma Bhalo na Abdilatif Abdalla. Hata hivyo, athari
za Muyaka hakuazimwa moja kwa moja na wafuasi wake. Kazi za watangulizi na
wafuasi wanaopatikana katika ujirani mmoja zinaweza kulinganishwa na
kulinganuliwa. Si hivyo tu; hata fasihi ambazo hazipatikani katika ujirani
mmoja zinaweza kulinganishwa.
M.S. Abdullah
na Conan Doyle wameandika masimulizi ya upelelezi. Abdulah anamfufua Sherlock
Holmes, nguli anayepatikana katika masimulizi ya Conan Doyle na kumweka katika
mazingira na muktadha wa Zanzibar. Isitoshe; Abdullah anakihamisha kipera cha
masimulizi ya upelelezi kutoka Ulaya hadi Afrika Mashariki. Kazi za Abdullah na
Doyle zinaweza kulinganishwa kwa msingi huo. Katika mkabala wa upelelezi kuna
wandishi wengine wa kipelelezi kama John Simbamwene, Faraj Katalambulla na John
Mtobwa wanaoweza kulinganishwa na kutofautishwa na mtangulizi wao, na vilevile
wao kwa wao.
Aina za athari
Kiwewe cha kuathiriwa
Baadhi ya
athari zinazowashughulisha walinganishi haziwezi kutambulika moja kwa moja.
Huwa zimejificha na hutaka uzoefu mkubwa wa uhakiki ili zitambulike na
kufichuliwa. Kwa hakika athari nyingine huwa kinyume na matarajio. Euphrase
Kezilahabi ni mwanafunzi wa Shaaban Robert. Kezihalabi amelelewa kwa hekima ya
shaaban. Amemsoma Shaaban na kuandika tahakiki nyingi juu ya Shaaban Robert
zikiwemo Ushairi wa Shaaban na Riwaya za Shaaban Robert.
Hata hivyo
katika ushairi wake na riwaya zake anaenda kinyume cha Shaaban Robert. Vilevile
kila mwandishi huyu anaposoma riwaya za Clara Momanyi hasa Tumaini na Nakuruto
pamoja na hadithi yake fupi, “Ngome ya Nafsi”, anakatikiwa kwamba kwa kiwango
fulani, Momanyi aliathiriwa na Kezilahabi kwa njia ya kipekee. Aliathiriwa kwa
kumkwepa na hata kumkosoa Euphrase Kezilahabi kwa mtazamo wake wa kukatiza tama
juu ya mtoto wa kike. Mhakiki Harold Bloom ameandika tahakiki ya ushairi
mashuhuri inayoitwa The Anxiety of
Influence ambapo anadai kwamba mwandishi chipukizi anapotaka kuwa maarufu,
lazima aepukane na sifa zilizomfanya mtangulizi wake kuwa mashuhuri na mtajika.
Kezilahabi anakuwa mtajika kwa “kufadhaishwa” na athari za Shaaban Robert.
Naye Clara
Momanyi anaendelea kupata umaarufu kwa kufaidhaishwa na athari za Euphrase
Kezilahabi. Jambo hili linakutikana katika fasihi za Kimagharibi nyingi.
Aristotle alikuwa mwanafunzi wa Plato. Wote walikuwa maarufu kwa njia tofauti
kwa sababu Aristotle alikwepa mkondo wa kutafakari wa Plato ijapokuwa
hakumkosoa mtangulizi wake moja kwa moja mtangulizi huyo akiwa hai. Katika bara
la Afrika wandishi kama Ngugi wa Thiong’o na Chinua Achebe wameathiriwa na
wandishi wa Kimagharibi kama Josef Conrad na W.B. Yeats mtawalia. Shujaa Okonkwo ni riwaya inayosomwa kwa
sababu za kifasihi, kianthropolojia, kidini na hata kisiasa. Kazi kama hii
inafaa sana kusomwa katika fasihi linganishi. Katika kitangulizi cha riwaya
hiyo, mtunzi anaonyesha kinaganaga kwamba amesoma kazi za kishairi za
mwanafasihi Yeats kutoka Ireland hasa shairi lake ‘The Second Coming’. Katika
‘The Second Coming’, Yeats anazungumzia matukio yanayosababisha kudidimia na
kupomoroka kwa utamaduni na ustaarabu wa Kimagharibi. Ustaarabu anaouhofia ni ule
uliojengeka kwenye misingi ya Ukristo, sayansi na teknolojia ya Kimagharibi.
Kwake sayansi na teknolojia ya Kimgharibi ni kilele cha juu cha maendeleo ya
mwanadamu. Ustaarabu huu unatishwa na ukafiri wa aina fulani.
Kiwewe cha
kuathiriwa kinatokea pale ambapo Achebe anatumia taswira na vitushi vya Yeats
ijapokuwa anayaweka malengo yake kichwamgomba. Ikiwa Yeats anatetea Ukristo na
sayansi katika shairi lake, Achebe naye anatoa madai kwamba Ukristo, sayansi na
teknolojia-zote asasi za mtu mweupe ndizo zimesababisha kudidimia, na
kubomolewa kwa ustaarabu wa Mwafrika. Kile kinachotetewa katika shairi la Yeats
kinageuzwa na kuwa kiashiria cha uovu na maangamizi katika jamii za Kiafrika.
Harold Bloom aliishilia katika kuorodhesha hatua ambazo mtunzi chipukizi angezipitia
ili apate umaarufu. Mwandishi huyu haamini kwamba lazima hatua hizo zote
zipitiwe ili chipukizi apate umaarufu.
Mwingiliano matini
Mwingilianomatini
ni dhana inayotumiwa kuezelea usemezano unaotokea kati ya sauti mbalimbali
zinazopatikana katika matini. Sauti zilizopo kwenye matini wakati huu zinaweza
kuwa mwangwi wa sauti za wakati uliopita, mwangwi wa sauti nyingine zilizopo na
zitakazokuja baadaye. Mwingiliano matini ni kitengo cha usemezano ambayo
kimsingi ni nadharia ya kiisimu jamii na fasihi. Katika isimu usemezano kwa
mujibu wa maelezo ya Mikhail Bakhtin uwezo wa sajili mbalimbali kuingiliana na
kusemezana kati yazo na vile kusemezana na misimbo ibuka kama msamiati mpya na
vilugha vya vikoa tofautitofauti katika jamii. Dhana ya mwingiliano matini
inaweza kuinuliwa kuwa kinadharia cha kuichangunulia fasihi linganishi. Mahali
ambapo matini zinaingiliana patadhihirisha mshabaha mkubwa kati ya kazi za
fasihi zinazolinganishwa.
Kinyume na haya
mahali ambapo matini zitatengana sana kimaudhui na kimtindo patathibitisha
tofauti zilizopo kati ya kazi za fasihi zinazohusika. Riwaya za Shaaban Robert
kama Adili na Nduguze na Kusadikika zinaweza kulinganishwa na
masimulizi ya Alfu Lela Ulela kwa
misingi ya mwingiliano matini. Muundo na usawiri wa ni mambo yanayoingiliana
hivi kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba kabla ya kuandika kazi zake Shaaban
Robert alikuwa amedurusu masimulizi ya Alfu
Lela Ulela. Mwangwi wa Alfu Lela
Ulela unasikika katika kila hatua ya kusoma Adili na Nduguze na Kusadikika
hususan tukizingatia Alfu Lela Ulela Kitabu cha Kwanza na Alfu Lela Ulela Kitabu cha Pili.
Mwingiliano matini ni mkabala unaofaa wa kulinganisha na kulinganua kazi hizi.
Riwaya ya Shaaban Robert ya Kusadikika
inaweza kulinganishwa na riwaya ya Katama Mkangi ya Walenisi kwa kutumia mkakati huu pia. Ingawa masimulizi ya Alfu Lela yanaweza kulinganishwa na
riwaya ya Walenisi, mshabaha
hautalingana na tofauti. Kuna viwango mbalimbali vya mwingiliano matini ambavyo
vinaweza kumsaidia mhakiki kujenga mihimili ya nadharia hiyo.
Athari katika Alfu Lela
Ulela: Kitabu cha 1(Kisa cha walii Wa 11 na mbwa wawili weusi)
Katika hadithi hizi mbili, inadhihirika wazi kuwa athari
ambayo imejitikeza moja kwa moja ni ile ya mwingiliano matini. Katika athari
hii inabainika wazi kuwa miangwi ya kisa kimoja inatoa mirindimo katika kisa
kingine ingawa mwandishi amejarubu kukwepa baadhi ya mifanyiko katika kila
mojawapo wa visa hivi.
Kwenye kisa cha Walii wa Pili yapo mazingira ya safari
inayopangiwa mwana wa Mfalme ambaye ameibuka gwiji wa elimu hasa dini na
kuandika Kiarabu. Sifa zake hizi zilimfanya sultan wa Bara Hindi kumtuma mjumbe
na zawazi ya utajiri kwa kumtaka mwanawe kuzuru kwa Mfalme wa Bara Hindi.
Miangwi ya safari vile vile inajitokeza katika kisa cha Mzee wa pili na Mbwa
Wawili Weusi. Hata hivyo safari hii ni ya tamaa za kibinafsi za Ndugu hawa
wafanyibiashara kwenda pwani kufanya biashara. Kwa hivyo safari hapa licha ya
ya kuwepo imepewa taswira tofauti.
Tukitazama
kwenye rasilmali, inaonekana wazi kuwa kwenye kisa cha Mbwa wawili, hazina
waliyo nayo hawa Ndugu wa watatu ni ya uridhi kutoka kwa baba yao ambaye kwa
sasa ni marehemu. Kwenye kisa cha walii wawili tunamwona Mfalme akiyatoa mali
yake kwa mwanawe ili ampelekee sultan wa Bara Hindi kama zawadi. Kwa hivyo
swala la asili ya mali na hela za matumizi kwa wahusika hawa linajitokeza
ingawa kwa ukinzani mkuu.
Swala
la mikosi ya safari zote hizi mbili limeangaziwa. Kwenye kisa cha mbwa wawili
weusi walendugu wawili waliotaka kauli ya kwenye kufanya shughuli zao za
kibiashara waliporudi hahi zao kama zinavyoelezwa na ndugu yao, hazikufurahisha
hata kidogo. Waliporudi walikuwa wanyonge na hali bin taabani na wamefilisika
pakubwa ishara kuwa huenda walishambuliwa na wazi na kuporwa kila walichikuwa
nacho. Kwenye kisa cha walii wawili, mikosi ya safari pia inajitokeza ambapo
mtoto wa Mfalme na ujumbe wake walipokuwa safarini, waliweza kushambuliwa na
wezi ambao walikuwa hamsini na kuwapora kila walichokuwa nacho licha ya
kuwateka nyara wajumbe waliokuwa wakisafiri na mwanawe Mfalme. Kwa upande wake
mwanawe Mfalme alipata kunusurika na kuhepana farasi wake ambaye alianga
kutokana na Jeraha alililipata katika uvamizi ule. Mwanawe Mfalme kwaupande
wake alijirusha nakuenda asikokufahamu mradi awe mbali na mikono ya wezi
watekaji nyara wasio na utu asilani.
Kwenye
kisa cha walii wa pili mwanawe Mfalme anapokea hisani kutoka kwa mshona viatu
baada ya kutaabika msituni akila matunda ambapo anapata hifadhi, maakuli pamoja
na zana za kujipatia riziki atakapokuwa katika nchi ile ngeni. Kwenye kisa cha
mbwa wawili weusi vile vile waathiriwa wa awali ambao ni ndugu wawili wanapata
hisani si kutoka kwa mtu wa mbali bali kutoka kwa ndugu yao ambaye aliwasihi
wasiende kwenye shughuli zao za kibiashara ingawa wakadinda. Kila mmoja
waoaliingia na maafa yake yaliyoandamana na kupunjwa kwa hela zao ikabidi ndugu
yao awakirimu kwa kila kitu sawa na alivyokuwa mshona viatu na mtoto wa Mfalme.
Wale
ndugu wawili waliweza kujifunza maswala yanayofungamana na biashara ambapo riziki
yao ya kucha kutwa walijikimu kwa kutumia jasho lao la kibiashara. Tukitazama
katika hadithi ya walii wa pili, mwanawe Mfalme hakuweza kujifunza
walakufundishwa kazi yoyote ya kiufundi ya kujikimi maishani bali alitegemea tu
wazazi wake. Hii ilidhihirika alipofika kwa mshona viatu ambaye alilazimika
kumpa shoka na kumshauri kuwa mchaja kuni.
Visa
vyote viwili vinaangazia swala la harusi katika mitazamo miwili tofauti kabisa.
Kwenye kisa cha mbwa wawili weusi, harusi ni ya hiari ambayo Ilipendekezwa na
jini kwenye umbo la binti mrembo. Harusi ile ilifungwa na wawili hawa
wakaabiri chombo wakiwa na nia ya kurudi nyumbani kuishi kama mke na
mume. Katika kisa cha walii wa pili, harusi iliyotarajiwa kati ya binti sultani
wa Kisiwa cha Mpingo na bin Sultani aliyekuwa binamu yake, haikufaulu kwani
binti aliwahiwa na jini la kiume ambalo lilimtia mateka na kumficha katika
makaoyake hayo ya ajabu.
Wahusika
hawa wote wawili wanapata hisani kutoka kwa wanawake wasiowafahamu kamwe.
Kwenye kisa cha mbwa weusi wawili mhusika huyu ananusurishwa na jini mfanowa
mwanamke wote wawili walipotupwa baharini ili wafe. Naye mhusika katika kisa
cha walii wawili anapewa hisani kutoka kwa mwanake mateka wa jini ambaye
anampamajiya kukoga, chakula na kumfariji kutokana na hali yake iliyokuwa ya
kusikitisha ajabu.
Kisa
cha Mzee wa Pili na Mbwa Wawili’, wanadamu wawili mbao walipanga njama ya
kumwua ndugu yao pamoja na mkwewe ambaye alikuwa jini wanabadilishwa na hilo
jini kama adhabu na kuwa mbwa wawili
weusi. Katika kisa cha walii wawili mhusika ambaye ni mwana wa Mfalme naye
anabadilishwa katika kiumbe cha kupaa angani nakujikuta amerudi pale pale
ardhini kwenye makao ya jini.
Ipo pia
ile hali ya kubadilika kwa mazingira kijini kiasi kwamba binadamu wakawaida
hawezi kutambua wala kubaini bayana. Kwenye kisa cha mbwa weusi, yule mtoto
aliyenusurishwa na jini alijikuta kwenye paa lake la nyumba ilhali walirushwa
baharini. Kwenye kisa cha walii wawili tunaiona hali kama hiyo ambapo jini
lajigeuza binadamu na kumjia mtoto wa sultani na kumtwaa kwa hali isiyoeleweka
na kujikuta kwenye makao ya jini.
Katika
kisa cha mbwa wawili weusi halikukubali yule binadamu aangamie walipotupwa
baharini hivyo likamwokoa kwa hali isiyoeleweka na mwanadamu wa kawaida. Katika
kisa cha walii wawili hapa mwanadamu ambaye nimkewe jini anamwokoa mtoto wa
sultani katika haili ya kawaida kwa kukataa kumwangamiza kwa silaha aliyopewa
na jini kwa kusema kusema kuwa hakuwa na nguvu za kushika upanga.
Mwingiliano
uliopo kwenye visa hivi viwili vile vile unaonekana kupitia kwa wahusika.
Katika kisa cha mbwa wawili weusi mwanamke anayemrai binadamu kumwoa ni jini na
hili linadhihirika wakati ambapo linamwokoa atupwapo baharini. Katika kisa cha
walii wawili nacho mwanamke anayemwokoa mtoto wa sultani si jini bali ni
binadamu wa kawaida aliyekuwa ametekwa nyara na jini.
Hitimisho
Kwa yakini
fasihi linganishi hasa athari ya mwingiliano matini imejitokeza waziwazi katika
visa hivi viwili kiasi kwamba mwandishi amekitumia kisa kimoja kukijenga na
kukikamilisha kisa kingine. Hata hivyo inaonekana kuwa kwenye kisa cha mbwa
wawili weusi mazingira ya kimwambao yanajitokeza dhahiri na kwenye kisa cha
walii wawili mazingaira hayana msabaha wowote na upwa. Wahusika nao vile vile
wameingiliana kwa njia moja hadi nyingine kulina na majukumu wanayoyatekeleza
kwenye visa hivi viwili.
Marejeleo.
Abdalla,
Abdilatif (1973). Sauti ya Dhiki. Nairobi:
Oxford.
Achebe, Chinua (1965). Morning Yet on Creation Day. London: Heinemann
Althuser,
Louis (1981). Ideology and Ideological
Apparatuses, Lenin and Other Essays
London: New Left Books
Aristotle
(1984 ) The Rhetoric. Trans. W. Rhys
Roberts. New York: Dover Publications.
Press
Bakhtin,
Mikhail (1981). The Dialogic Imagination.
Austin: University of Texas Press.
Bakhtin,
Mikhail (1984). Problems in Dostoevsky’s
Poetics. Manchester: Manchester University
Press.
Bakhtin,
Mikhail (1986). Speech Genres and Other
Late Essays. Austin: University of Texas
Press
Dan, Ben-Amos (1977). Folklore Genres. Bloomington: Indiana University Press
Bloom,
Harold (1973) The Anxiety of Influence.
New York: Oxford University Press.
Gifford,
Henry (1969). Comparative Literature:
Concepts in Literature. London: Routledge
& Paul Kegan
Habwe,
John (2008). Cheche za Moto. Nairobi:
Jomo Kenyatta Foundation.
Harries,
Lyndon (1962). Swahili Poetry.
Oxford: Clarendon Press.
Hichens,
William (1972). Al Inkishafi.
Nairobi: Oxford University Press.
Kareithi,
Peter (1969) Kaburi Bila Msalaba. Nairobi: East African Publishing house.
Kezilahabi,
Euphrase (1971). Rosa Mistika.
Nairobi: Kenya Literature Bureau.
King’ei,
Kitula (2007). ‘Athari za Washairi Wakongwe juu ya Washairi wa Kisasa:
Mfano
wa Muyaka Bin Haji na Ahmad Nassir’ Kioo
Cha Lugha. vol 5 (30-38). Dar es Salaam: Idara ya Kiswahili.
Lukacs,
Georg (1962). The Historical Novel.
Lincoln: Nebraska University Press.
Mkangi,
Katama (1995). Walenisi. Nairobi:
East African Educational Publishers
Mkangi
Katama (1984). Mafuta. Nairobi: East
African Educational Publishers.
Mlamali,
Hamad (1980). Inkshafi: Ikisiri.
London: Longman.
Mohamed,
Suleiman (1976). Nyota ya Rehema.
Nairobi: Oxford.
Mohamed,
Said Ahmed ( 2001). Babu Alipofufuka.
Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation
Mohamed,
Said Ahmed (1980). Dunia Mti Mkavu.
Nairobi: Longman
Momanyi, C. Tumaini.
Nairobi: Vide~Muwa Publishers Limited,
2006.
Mulokozi,
Mugyabuso (1979). Mukwava wa Uhehe.
Nairobi: East African Publishing House
Ngare,
J (1974). Kikulacho ki Nguoni Mwako.
Nairobi: East African Publishing House.
Orwell,
George (1967) Shamba la Wanyama. Taf.
ya Kawegere. Nairobi: East African
Publishing House
Shafi,
Adam (1978). Kasri ya Mwinyi Fuad.
Dar es Salaam : Tanzania Publishing House.
Sofokile,
(1969) Mfalme Edipode. Nairobi:
Oxford
Valdes,
Mario et al (1992). Comparative
Literature as Discourse. Bern: Berlin: Peter Lang
Wafula,
Richard Makhanu (1999) Uhakiki wa
Tamthilia: Historia na Maendeleo Yake.
Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation