HAKIKI MAUDHUI YANAYOJITOKEZA KATIKA MIMBA INGALI
MIMBA NA HADITHI NYINGINE (MC ONYANGO,2006).
Maana ya Maudhui
Kwa upande wa maudhui imekuwepo mikinzani na mikanganyiko nuongoni
mwa wanataaluma wa kazi za fasihi juu ya maana yake. Wengi wa wananadharia hao
wanajadili fani na maudhui pamoja, japo pengine mitazamo yao haiwi sahihi.
Baadhi ya wanataaluma wa kazi za fasihi wanasema kwamba fani na
maudhui ni vipengele ambavyo havina uhusiano wowote na kwamba vinaweza
vikatenganishwa. F.V. Nkwera analinganisha fani na maudhui na
kikombe na maji. Kikombe kinachukuliwa kama ndiyo fani, na upande mwingine maji
ndiyo maudhui. Mnywaji wa maji hayo analinganishwa na msomaji wa kazi ya
fasihi.
S.D.Kiango na T.S.Y.Sengo wanafafanua fani na
maudhui kwa kulinganishwa na chungwa ambalo lina sehemu ya nje na ndani.
Maudhui ya kazi ya sanaa yanalinganishwa na nyamanyama za chungwa na fani ni
ile sehemu ya nje.
Mawazo mengine juu ya fani na maudhui yanatolewa na Penina Muhando
na Ndyanao Balisidya ambao wanaelekea nao kuukubali mtazamo huu ulioelezwa hapo
juu wakati wanapoelezea hadithi kuwa na "umbo la nje" wakati lugha
inapotumiwa na kujenga hilo umbo la ndani (maudhui) ambalo huhusika na wazo kuu
analolitaka fanani, (dhamira) ujumbe wake, maadili, na falsafa zake (kama zipo)
za maisha."
Nadharia hizo zote zilizojadiliwa hapo juu kwa ujumla zinaonyesha
kupwaya na zinaweza kuwakanganya wasomaji. Nadharia hizo hazionyeshi ama
kuwakilisha ukweli wa mambo ulivyt) juu ya uwiano uliopo kati ya fani na
maudhui katika kazi ya sanaa kwani zinaonyesha kuwa fani na maudhui ni vitu
viwili vinavyoweza kutazamwa katika utengano, jambo ambalo si la kweli. Ukweli
ni kwamba vitu hivi viwili vinategemeana na kukamilishana, na wala havitazamwi
katika utengano.
Ufafanuzi wa kuiona fani na maudhui kama kitu kisichoweza
kutenganishwa umefanywa na Henri Arvon, Avner Zis na wanataaluma wengine
wengi walio na mtazamo wa kisayansi ama kiyakinifu.
Kwa upande wa fasihi ya Kiswahili, M.M. Mulokozi na K.K. Kahigi
wamekuwa na mtazamo wa aina hiyo pia. Wanafasihi hao wanasisitiza kuwa
"fani na maudhui huathiriana na kutegemeana ... Maudbui ni maana ya shairi
(kazi ya sanaa), ni yale mawazo yanayozungumzwa (dhamira, falsafa, maoni),
pamoja na mtazamo wa mtunzi juu ya mawazo hayo... wazo kuu (dhamira) na mtazamo
wa msanii hutupa ujumbe."
Akiungana na mtazamo huu, Senkoro naye anasema kuwa "maudhui
ni jumla ya mawazo, mafunzo yapatikanayo katika kazi ya fasihi... Maudhui
huunda lengo kwa mwaudishi. Kutokana na lengo, mawazo na mafunzo ya mwandishi
ndipo tunapata falsafa. Mawazo, mafunzo, lengo na falsafa au mtazamo wa
mwandishi kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii huunda msimamo."
Mawazo hayo aghalabu yanajaribu kufafanua nini hasa ni maudhui.
Lakini dhana ya kutotenganishwa kwa vitu hivi viwili haijawekwa waziwazi. Ndipo
Senkoro anapotumia mfano wa "sarafu" kwa kufananisha fani na maudhui
ya kazi ya sanaa na "sura mbili za sarafu moja." Mfano huu
unajaribu kusisitiza dhana ya kutotenganishwa kwa fani na maudhui katika kazi
za sanaa za kifasihi. Mfano huu wa sarafu unajaribu kuonyesha dhana ya
ukamilifu ya fani na maudhui kama kitu kimoja cha kazi ya sanaa kwa kutumia
mfano wa sarafu yenye sura mbili, lakini umuhimu wake kama sarafu moja
unategemea tuweko kwa sura hizo mbili. Sura moja ya sarafu ikikosekana, basi,
sarafu hiyo haiwezi kuwa na hadhi yake ya kisarafu. Jambo la muhimu ni kuona
jinsi kitu kimoja (fani) kinavyoweza kukikamilisha kingine (maudhui).
Kwa kuzingatia nadharia hizo, tunakubaliana na Senkoro au
Mulokozi na Kahigi wanaosema kuwa "fani na maudhui
huwiana, hutegemeana na hatimaye kuathiriana." Uhusiano huu ndio unaojenga
kazi bora ya fasihi. Aidha ni vizuri kutoa tahadhari hapa kuwa uwiano wa fani
na maudhui wa kazi ya sanaa huwa ni lengo la msanii. Maudhui iliyotawala
kuumbwa kwa kazi ya sanaa inatakiwa kujitokeza katika fani inayohusu. Ili
maudhui yatawale fani, sharti yajitokeze kama kazi ya sanaa na si kama hotuba
ya mwanasiasa. Ni wajibu wa msanii kuchagua fani inayomruhusu kutumia maudhui
anayotaka kuyafikisha kwa hadhira yake.
Vipengele vya maudhui ni pamoja na dhamira, migogoro, falsafa
ujumbe na msimamo.
1.
Dhamira; hili ni wazo kuu au mawazo mbalimbali yanayojitokeza katika
kazi ya fasihi. Dhamira ni sehemu tu ya maudhui na aghalabu dhamira kuu ndio
hujenga kiini cha kazi ya fasihi. Dhamira zimegawanyika katika makundi mawili,
kuna dhamira kuu na dhamira ndogondogo.
2.
Migogoro; hii ni mivutano na misuguano mbalimbali katika kazi za fasihi.
Migogoro inaweza kuwa kati ya wahusika, familia zao, matabaka yao, au hata
katika nyadhifa mbalimbali. Vilevile migogoro yaweza kuwa ya kiuchumi, kijamii,
mogogoro ya nafsi, na migogoro ya kisiasa ambayo hujitokeza katika mitazamo
tofauti kulingana na mtiririko wa visa na matukio yanavyopangwa na mwandishi.
3.
Ujumbe; mwandishi anapoandika kazi yake huwa na ujumbe ambao hutaka
uifikie jamii aliyoikusudia. Ujumbe katika kazi fasihi ni mafunzo mbalimbali
ambayo hupatikana baada ya kusoma kazi ya fasihi. Katika kazi ya fasihi dhamira
kuu hubeba ujumbe wa msingi na dhamira ndogondogo hubeba ujumbe ambao husaidia
kuujenga au kuupa uzito zaidi ujumbe wa msingi.
4.
Msimamo; katika kazi ya fasihi, mawazo, mafunzo na falsafa ya msanii
hubainisha msimamo wake kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii. Msimamo ni ile
hali ya mwandishi kuamua kufuata na kushikilia jambo fulani. Jambo hili huweza
kukataliwa na wengi lakini akalishikilia tu. Msimamo ndio huweza kuwatofautisha
wasanii wawili au zaidi wanaoandika kuhusu mazingira yanayofanana. Kwa mfano,
katika tamthilia ya “Pesa zako zinanuka” mwandishi anamsimamo wa kimapinduzi
kwani amejadili matatizo yanayochangia kukwama kwa ujenzi wa jamii mpya.
5.
Falsafa ni mawazo ya busara yenye kutawaliwa na misingi mahususi
juu ya asili na maana ya ulimwengu na maisha ya mwanadamu. Ni msimamo wa msanii
katika maisha juu ya utatuzi wa matatizo katika jamii. Falsafa ya mwandishi
inaweza kujulikana kwa kusoma kazi zake zaidi ya moja.
6.
Mtazamo ni hisia au uelewa wa mwandishi juu ya jambo fulani. Kwa
mfano anaweza kutazama jambo fulani kwa mtazamo wa kidini, au anaweza kutazama
jambo fulani kwa mtazamo wa kisiasa au kisayansi.
7.
Mafunzo; ni mawazo ya kuelimisha yanayopatikana katika dhamira
mbalimbali za kazi ya fasihi.
Uhakiki wa Maudhui katika Mimba
ingali mimba na Hadithi Nyingine
KJwa kweli huu ni mkusanyiko wa
hadithi ambazo moja kwa moja zinaiafiki jamii ya sasa. Mhariri ameziteua
hadithi hizi kwa ustadi ili kulitimiza lengo lake katika jamii. Maudhui haya
yamejiratibu ifuatavyo kutoka hadithi moja hadi nyingine.
Bimdogo Selina
Elimu
Maudhui
ya Elimu yamejitokeza wazi wazi katika hadithi hii. Tunakumbana na Selina
ambaye anaishi na Shangazi yake kwa jina Shefsa. Hali ya masomo ya Selina
inaingia mchanga kwani hapewi mazingira mazuri ya kumwezesha kusoma akiwa na
Utulivu.
Selina
huamshwa asubui na mapema akakoga na kuondoshwa halahala kabla hata ya
kuimaliza chai yake ili aende shuleni kwa kupitia sehemu fulani za kisiri
ambazo yeye mwenyewe hakuweza kufahamu mzigo aliokuwa akipewa kumpelekea
Kionyeshaa kila asubui.
Sare
yake ya shule haitamanishi pamoja na vyatu vyake ambavyo hali yake inatia hofu
na mashaka.
Kwa
kweli elimu kwa mtoto wa kike bado ni changamoto kiasi katika baadhi ya jamii
zetu za Kiafrika. Hii ni kutokana na mila ambazo zimepitwa na wakati pamoja na
taasubi za kiume kuwa mwanamke hafai kwa lolote wala chochote.
Matumizi ya Mihadarati- dawa za kulevya
Kila
asubui Selina anaoondoka kwenda shuleni, Shangazi yake alikuwa akimpa kijimzigo
kidogo kukifikisha kwa Kionyeshaa. Mwanzoni hakufahamu hadi alipotiwa mbaroni
na polisi walienda Usalama. Tunazidi kuona namna jamii kwa kupitia wateja wake
Kionyeshaa inavyoathirika na matumizi ya mihadarati.
Dhuluma kwa watoto wa kike.
Kupitia kwa maisha ya Srlina na
Shangazi yake, inadhihirika wazi kuwa mtoto wa kike anakumbwa na vizuizi vingi
mno katika maisha yake. Wanapewa majukumu hatari yanayoweza kuwatika Mashakani
na hatarini.Kwa mfano Selina alikuwa akitimiwa katika usafirishaji wa dawa za
kulevya kutoka kwao nyumbani hadi kwa Kionyeshaa. Licha ya kutumiwa kama mrija
wa kitega-uchumi, Shangazi yake hamshughulikii katika maswala ya kimsingi kama Mavazi, chakula n,k..
Mimi Sijui
Uramali/Uganga/Usihiri
Katika
jamii husika inathibitika wazi kuwa watu wanathamini sana Mazingaombwe kuliko
maswala halisi.Hii inathibitika wakati wakazi hawa wamesusia kutazama mechi ya
mpira uwanjani ili waweze kutazama Mazingaombwe yanavyoendelezwa. Wanastajabia
mabadiliko ya vitu asilia kutoa vitu vingine kabisa.
Ulevi
Maudhui
haya yanajitokeza kupitia kwa mhusika Hamsini Zangu ambayo daima yuko mbioni
kutafuta mteja wa kukinunua alichonacho ili apate hela za kununua kileo. Baada
ya muda mfupi, bwana huyu anatokeza akiwa mlevi chakari hajijui hajitambui.
Uchachu huja Baadaye
Elimu
Hii ni hadithi ambayo Waaidha imeangazia
swala la elimu. Tunakumbana na wahusika mbalimbali wakiwa katika mazingira ya
elimu. Hawa ni pamoja na Moronya na Kimbo. Wawili hawa wako katika awamu ya
mwisho katika chuo ambapo wanasomea utabibu.
Ukengeushi
Hali hii imedhihirika kwa wahusika mbalimbali ambao
kinyume na lengo lao masomoni, hujkubali kunaswa na ufuska fulani. Baadhi ya
wahusika hawa ni pamoja na Moronya ambaye amewajaza wasichana kwenye mwili kama
Mavazi huku wakipokezana zamu katika chumba chake cha malazi.
Ufuska huu haukukomea hapo chuoni bali hata baada ya
kudarijiwa na akaanzisha zahanati ndogo mjini Nakuru na rafiki yake, tunamwona
akizidi tu kuzama katika Usherati kwa kuwavizia wake za watu ambao huja kwake
roho safi wakihitaji huduma za kiafya. Vitendo vyake hivi ndivyo
vilivyomwingiza kaburini huku akiwa na majuto chungu nzima.
Ukimwi
HIV (VVU) ni mdudu mdogo sana,
inajulikana ka virusi, kwamba huwezi kuona. UKIMWI (Upungufu wa Kinga Mwilini)
ni ugonjwa ambao unaendelea baadaye, baada ya mtu kuambukizwawa virusi vya
UKIMWI.
Mtu hupata
UKIMWI wakati mfumo wa kinga unapokuwa dhaifu na kushindwa kupigana na
maambukizi. Mara nyingi dalili ni; Kuwa mgonjwa kwa muda mrefu na magaonjwa ya
kawaida kama vile kuhara au mafua. Dalili za UKIMWI zinaweza kuwa tofauti
kutoka kwa mtu mwingine hadi mwingine. Mtu aliye na UKIMWI anaweza kupata
maambukizi ya magonjwa amabayo huwa nadra kwa wasio na virusi vya ukimwi, kama
baadhi ya saratani au maambukizi ya ubongo.
Lishe bora na madawa yaweza kusaidia mwili
kupambana na maambukizi na kukumuwezesha kuishi kwa muda mrefu. Lakini hakuna
tiba ya virusi vya ukimwi.
Janga hili limekuwa tisho kubwa katika jamii
zetu. Watu hufa kucha kutwa bila hodi wala karibu. Hapo tunakumbana na Moronya
ambaye tabia zake za Uasherati zinamsababishia gonjwa la ukimwi ambalo
linamwanamiza. Hali yake hii inaweza kuafiki methali, “ Mwanamaji wa kwale kufa
maji mazoea”
Majuto
Maudhui haya yanajitokea kwenye
wahusika mbalimbali. Mkewe Moronya anabaki pweke katika bahari ya majito kuhusu
kifo cha mumewe akikosa kujua namna ya kuijenga na kuiendeleza jamii. Kwa
upande mwingine, Moronya naye anajutia matendo yake ya ufuska anapokuwa katika
hali zake za mwisho duniani. Wazazi wake Moronya nao hawakusazwa. Hawa walikuwa
na ndoto ya kupata mtoto ambaye angekuwa tabibu ili kuiokoa jamii. Maombi yao
hayakuwa na chochote wala lolote walipogundua kuwa mwanao alikuwa ameambukizwa
maradhi ya ukimwi na hali yake ilikuwa taabani ambapo mauti yalimkodolea macho.
Jeraha
la Raha
Uasherati
shannie na Dabbo ni makahaba ambao wanajiuza na wakinaswa
wanatumia ngono na polisi kama malipo ya kuwawacha wenzao walioshikwa huru ale
polisi waotawaliwa na kasumba hii wanadhihirika kupitia kwa inspekta Karama.Ulafi
wa kimapenzi wa Karama ndio unaomletea fedheha.
Mihadarati
Shannie anajitokeza kama mtumizi
hodari na hatari wa dawa za kulevya. Hii inadhihirika wazi anapowawacha Dabbo
na Mnaziri katika hoteli ya Beach View Kunduchi, anaenda kwake kupanga mikakati
ya kazi yake . Tunamwona Shannie
akimhadaa Karama ili wakutane kwa mahaba kumbe ulikuwa ni mpango wa kumtia dawa
za kulevya ili Karama aabike kupita kiasi. Hili Shannie alilitekelezeakatika
chumba na,bari 28 kwenye hoteli ya kimataifa ya Sea line ambayo ipo ufukweni
mwa Bahari ya Hindi eneo la Oysterbay.
Kisasi
Shannie anapanga kisasi kwa Karama
kwa swala la kuwadhulumu kimapenzi wanawake ambao waume zao walikuwa wameitwa
mbaroni. Hili alilitekeleza kwa wepesi sana kutokana na tamaa ya kimapenzi
aliyonayo Inspekta Karama.Alilitekeleza hili kwa wepesi mno na hakupatikana
popote na wale wote walikuwa washukiwa, waliachiliwa kwa kukosa ushahidi wa
kutosha. Shannie kwa upande wake akabaki salama wa salmin.
Unafiki
Inspekta Karama anatiwa shimiri na
Shannie na kumfanya Karama kutenda kwa kazi yake na wenzake kule Morogoro
kufanya uchunguzi kuhusu mauaji yaliyotokea katika eneo la Msamvu. Alipiga
bongo na Shannie ili awadanganye wenzake kuwa ameshikwa na Ugonjwa wa ajabu wa
kuanguka maruhani. Hii ilikuwa tu mbinu ya kupata muda mwafaka wa kukutana
kimapenzi na Shannie pasi kujua yaliyomngoja mbeleni.
Siri ya
Mama
Ustahaimilivu
Maulidi alivumilia kukaa na (Rehema) mkewe kwa muda wa
miaka minane bila ishara yoyote ya kupata mtoto.
Rehema alivumilia tabia za Maulidi kulala nje kwa mkewe
mpya mtakiwa bila kuteta hata siku moja.
Ukewenza
Mke mpya kutaka Maulidi amwache mkewe wa kwanza kwa kuwa
alionekana kuwa tasa.
Mke wa pili kumshauri wa tatu kuimba wimbo wa kuachwa kwa
mke wa kwanza.
Tamaa
Maulidi kutamani kuwa na watoto kutoka kwa Rehema
Rehema kutamani mumewe akubali kupimwa
Maulidi kuzidi kuwa na tamaa ya mtoto wa kiume baada ya
mkewe wa pili kudinda kuzaa tena baada ya kumzalia watoto watatu wote
wasichana.
Umdhanaye ndiye kumbe siye.
Maulidi ndiye aliyekuwa na matatizo ya kizazi kinyume na
alivyojijua.
Rafiki yake Maulidi kumpa ushauri ambao hauna msingi
wowote.
Rehema kudhaniwa tasa kumbe la.
Mke wa pili kudhaniwa kuwa mwaminifu kumbe ni mcheza
kando.
Siri
Wale wanawake wa pili na wa tatu
wanafanya siri ya kuwazaa watoto nje ya ndoa huku wakimdanganya Maulidi kuwa
yeye ndiye baba halisi wa watoto wanaozaliwa.
Rehema anaakubali kuiweka siri ya
hali halisi ya Maulidi hata baada ya kufichuka kuwa Maulidi ndiye aliyekuwa na
matatizo ya kizazi ambapo risasi alizizitoa hazikuweza kuua.
Siri ya hali ya kasoro ya Maulidi yafichuka alipokubali kupimwa ili
kuthibitisha ukweli halisi ulipokuwa.
Sitaki
Usaliti
Franklin anasaliti uhusiano wake na kimwana ambaye
alimhadaa hapo awali-Nyamweko.
Uraibu
Wawili hawa walikuwa waraibu wakubwa
wa kupiga mtindi katika mwanzo wa uhusiano wao hali ambayo Nyamweko
anailalamikia wakati wanapokosana. Anasema kuwa kila mara waliporudi usiku
wakiwa walevi jambo ambalo liliwaudhi wazazi wa Nyamweko.Uraibu huu ulijumlisha
ufanyaji wa mapenzi kiholela ambapo Nyamweko aliweza kupata uja uzito ambao
Franklin alimkana kwa kinya kipana.
Mjuto
Vijana wanaojiingiza katika mapenzi ya mapema hujikuta
wakijutia uamuzi wao huo. Nyamweko anajutia natendo yake ya kuwadharau wazazi
wake kwa kufumbwa macho na mahaba kati yake na Franklin.
Uchungu wa mwana
Mamaye Nyakwemo alimtetea kila mara aliporudi nyumbani
akiwa mlevi na Franklin hali ambayo ilimsababishia kichapo kutoka kwa babaye
Nyakwemo.
Alipofukuzwa kwa mpenzi wake, alikaribishwa na mamaye
ambaye alimsamehe kisha kumpa vifungu vya Bibilia kama kumpa moyo na imani.
Alichukua fursa vile vile ya kumwombea msamaha kwa babake.
Uasherati
Vijana wa kiume wakiwakilishwa na kina Franklin,
wanajiingiza katika maswala ya usherari ambapo wanakuwa na tabia za kuwaringa
mimba wasichana wasiokuwa na ufahamu wa kimaisha. Pindi wanapowatinga mimba,
hawawajibiki kwa lolote huku wakiwakashifu wahusika kuwa malaya.
Matendo maovu ya vijana hawa
yanashinikizwa na wazazi wao hasa baba zao ambao wanawapa vichwa vigumu vya
kuzikana mimba hizi pindi zinapotokea. Hawaonekani kuwajibikia matendo yai
maovu bali wanawawachia wasichana hawa kujishughulikia wenyewe kabisa.
Mimba
Ingali Mimba
Tamaa na matumaini
Nekesa alikuwa na tamaa na matumaini ya
kuitwa mzazi ingawa kila kuchao hali hubakia vile vile. Tamaa yake hii
inabaki kitendawili kwani hadithi inapokamilika hali yake inabaki vivyo hivyo
akisubiri heri ambayo haijui itakapofika.
Mila na tamaduni
Katika hali yake ya uja uzito,alijikuta akisghulikiwa
kadri jamii ilivyotaka hasa wakati mwanamke awapo na uja uzito.
Waliohujumu
ujamaa
Mauti/Mauko
Hadithi inaanza na kifo cha Fisi ambaye alikuwa Ndugu
yake ingawa hakikuwa kifo kamili bali mtego tu wa kutimiza kiu chake cha kula
nyama za wenziwe.
Uroho
Binadamu kurithi na kumiliki takribani kila kitu huku
viumbe wengine wakitaabika kwa kukosa riziki.
Ananyemelea mbuga la wanyama, kukatwa kwa miti kwa wingi.
Kusababisha kukauka kwa vyanzo vya maji vilivyosababisha
mito kukauka.
Ujamaa
Wanyama kukusanyika katika kuomboleza kifo cha fisi.
Kumboleza kwa mtindo kipekee na kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa
majukumu.Ngri kuongoza shughuli za mazishi.
Fisi kuijenga nyumba kubwa akiwana lengo la jamaa zake
kupata mahali pa kupumzikia na kulala wanapomtembelea.Hakutaka wengine
kulazimika kukaa nje kwa ukosefu wa nafasi.
Ulafi
Inadhihirika wazi kuwa Fisi kama
anavyojilikana kuwa mlafi, alijijengea nyumba yake kubwa kama kisingizio cha
udugu na ujamaa kumbe alikuwa na mpango wake fiche. Hii iligunduliwa na Sungura
mbaye ni kakake alipokuwa akiuchungunguza ule mwili wa Fisi na kukosa kuona
ukiwa wa mfu bali umelazwa kwa silaha kali. Walipokuwa katika maombolezo
kamili, Fisi alitokeza na kuwaua wale wanyama wote kwa kutumia vifaa alivyokuwa
amevilalia.
Mji wa
New York
Ubaguzi
Hili linajitokeza katika hotuba iliyotolewa
na Adu Emeka katika ukumbi wa mikutano kwenye Umoja wa Mataifa. Hotuba yake
ilionyesha kupinga vikali namna visa vya ubaguzi vilivyotanda katika nchi
mbalimbali zikiwemo Mashariki ya kati, Zimbabwe, Namibia na Afrika Kusini
ambako ubaguzi wa rangi ulikuwa umekita mizizi. Wamarekani halisi hawawatambui Wamarekani weusi ingawa hao weusi
ndio walioshika uchumi wa taifa hilo.
Unafiki
Licha ya Wamarekani kujifanya wanapinga
ubaguzi wa rangi kule Afrika Kusini ilhali hawakuwa wakifikiria unyama wao
nyumbani wa kuwanyanyasa na kuwabagua Wamarekani wenye ngozi nyeusi.
Uhayawani
Yule bwana aliyekuwa amevalia suti yenye
manyoya ya kondoo alijifanya kuwa mwelekezi wa balozi kumbe ni mhalifu na
mnyang’anyi mkubwa. Alimpiga balozi kabari na kumwonya kuwa iwapo angepiga
ukelele basi angekiona cha mtema kuni.
Alimnyang’anya balozi kila senti aliyokuwa
nayo akitishia kumwua.
Licha ya kuibiwa hela zake Balozi anapofika
kwenye kituo cha kukatia tiketi ya gari , yule mkata tiketi hakuta kumsikiza
hata kidogo na kumjibu kwa ujeuri kabisa.
Visa vya utekaji nyara na mauaji kiholela
vimetanda katika mji wa New York kiasi kwamba hata wengine ambao ni wamerika
huwaua watu kama njia moja ya kujifurahisha.
Usherati
Ni imani ya wakazi wa eneo atokako Balozi
kuwa vifo vingi vya wanaume huwa mikononi mwa wanawake. Hii ni kwa sababu
wakati balozi anapokuwa taabani, mwandishi anasema kuwa watu wa kwao wangeamini
kuwa alikufia mikononi mwa mwanamke fulani.
Kasheshe
jijini
Mauti/Maangamizi
Mlipuko wabomu ambao uliwaacha wengi wakiwa
hoi katika bomu lilitegwa kwenye ubalozi wa Merikani jijini Nairobi Waliobaki
kwenye matatu aliyosafiria msimulizi waliangamia kwa kuwa msimulizi anasema
kuwa aliiona matatu ile ikiteketea.Watu wengi waliweza kuaga dunia akiwemo
mhusika Rose.
Ujamaa
na udugu
Wananchi walijitolea kuwasaidia waathiriwa wa
mkasa huo wa bomu pamoja na vikosi mbalimbali vya Wanajeshi vilivyowasili ili
kufanya uchunguzi pamoja na kuwaokoa waliokuwa wamekwama kwenye vifusi vya
jingo hilo.
Mganga
wa Tanga
Kutowajibika
Mamaye Dalo alimsubiri Daktari wa mchana kutoka alipoenda
kupata kishuka bila ufanisi wowote. Daktari yule hakurudi kamwe. Ilipofika
usiku takriban saa moja na nusu ndipo Daktari wa usiku alipofika.
Uganga
Jamii ya kina Dalo umeamini sana katika swala zima la
uchawi. Hii inatokana na imani kuwa ni mganga tu ambaye angeweza kumtibu mtoto
wao kutokana na Ugonjwa wake wa ajabu.
Kisasi
Jamii ya kijana aliyeiawawa na Dalo
walipososana kwenye pilkapilka zao, alifanya Mazingaombwe ya kimila ili
kuhakikisha kuwa wanalipiza kisasi.
Tamati
Hadithi katika kitabu cha hadithi fupi
zinaingiliana moja kwa mojakatika maudhui. Hali hii inajitokeza waziwazi
kwanzia kwenye hadithi tangulizi hadi tamatisha. Imejitokeza wazi kuwa maswala
ibuka katika jamii za kisasa kama matumizi ya mihadarati, unyanyasaji wa mtoto
wa kike , mila na tamaduni zilizopitwa na wakati, taasubi ya kiume,ujamaa na
udugu yamejiweka wazi.
Kupitia kwa haya, waandishi hawa walikuwa na
nia na madhumuni ya kuipa mwangaza jamii kuhusu hali halisi ya maisha na namna
ya kulikabili hali hiyo.
Marejeleo
a.
Njogu, K. & Chimerah, R (1999): Ufundihsaji wa Fasihi: Nadharia na Mbinu.Nairobi: Jomo Kenyatta foundation.
b.
Mohamed,S.A. (1995): Kunga za Nathari ya Kiswahili. Nairobi: Oxford
c.
University Press.
d.
Wamitila,K.W. (2002): Uhakiki wa Fasihi: Misingi na Vipengele Vyake. Nairobi:Phoenix Publishers Ltd.
e.
Balisidya, M.L. (1987): ‘Tanzu na Fani za Fasihi simulizi’ katika MulikaNa 16. Dar es Salaam: T.U.K.I.
f.
Njogu, K. & Chimerah, R. (1999): Ufundishaji wa Fasihi: Nadharia na
g.
Mbinu Nairobi: J.K.F.
h.
Mazrui, A.M. & Syambo, B.K. (1992): Uchambuzi wa Fasihi. Nairobi:
E.A.E.P.
i.
Sengo,T.S.Y. (1987):Fasihi Simulizi: Sekondari na Vyuo Dar-es Salaam Nyanza Publications Agency.
j.
MCOnyango,
O(Mh)-2008: Mimba Ingali Mimba na hadithi
nyingine. Nairobi,Focus Publishers Ltd