Monday

kufafanua dhana za utafiti

0 comments

 

ELEZA KWA KINA DHANA ZIFUATAZO:

1)       Usuli

Usuli wa utafiti ni kile ambacho kimempa msukumo mtafiti kuifanya kazi yake. Waaidha huwa ni maelezo mafupi yanayohusu historia fupi kuhusu suala la utafiti ambalo unanuia kulifanyia utafiti.

Kwa mfano ikiwa mtafiti angenuia kufanya utafiti kuhusu sababu za wanafunzi wa eneo la pwani kutoweza kufanya vizuri katika somo la Kiswahili kwenye mtihani wa kitaifa, basi mtafiti husika hana budi kuyafafanua haya kuhusu Usuli wa utafiti wake kuhusu mada yake:

Kiswahili ni mojawapo ya lugha za mawasiliano nchini Kenya, ikiwa lugha rasmi ya kitaifa. Kuna malalamishi kuwa chimbuko la lugha ya Kiswahili ni upwa wa Afrika Mashariki (Massamba 2001), likiwemo eneo la Mkoa wa Pwani, nchini Kenya.Tume ya Elimu ya Gachathi 1976, ilipendekeza kuwa Kiswahili liwe somo la lazima kisha litahiniwe katika shule za msingi na za upili.

Nayo Tume ya Elimu ya Mackay 1981, ikatekeleza pendekezo la Tume ya Elimu ya Gachathi 1976 katika mfumo wa elimu wa 8-4-4. Kufikia sasa, ni zaidi ya miongo miwili tangu Kiswahili kilipoanza kutahiniwa katika kiwango cha kitaifa, kukiwa bado kuna madai kwamba matokeo ya mitihani ya Kiswahili ya K.C.P.E na K.C.S.E yamekuwa mabaya na yanaendelea kuwa mabaya. “Matokeo ya wanafunzi katika Kiswahili hayaridhishi. Kazi ya wanafunzi hasa katika insha za Kiswahili ilionyesha tofauti ndogo sana kutoka kwa ile ya mwaka wa 1989.”

Katika Usuli mtafiti anaweza vile vile kurejelea utafiti wa Mashirika au watu mabalimbali kama Kichocheo cha kumwezesha kuufanya utafiti wake.Kwa kulishughulikia hilo huwa ni ithibati tosha kuwa mtafiti anafahamu panda-shuka zote katika uwanja anaotarajia kutafiti.

2)      Swala la utafiti.

Hili huwa ndiyo mada au pengo ambalolinatarajiwa kuzibwa katika utafiti husika.

Kwa nini kuwe na swala la  utafiti?

-          Ikiwa watu wanazidi kuongelea juu ya swala hilo.

-          Kwa kuiangalia tu kama mtafiti.

-          Hutokea pale ambapo mtu binafsi au kiwanda Fulani kinazidi kuwa na matatizo

-          Mada ya utafiti hutokea plale ambapo kuna njia mbili ambazo zinahitajika kusuluhisha shida/tatizo hilo.

JINSI YA KUTEUA MADA YA UTAFITI

Mugenda na Mugenda, Research Methods (1999) wanasema mchakato wa utafiti huanza kwa kuchagua mada ya utafiti na hili huwa jambo tata kwa wanafunzi na hata watu ambao wamebobea katika uwanja huu wa utafiti.

Swali unalopaswa kujiuliza ni je nataka kutafiti kuhusu jambo gani? (Hiyo ndiyo mada) hii ni kwa sababu mada kamilifu yapaswa kujitosheleza na kulenga tatizo maalum lenye mipaka halisi. Haifai iwe pana wala finyu bali iwe wastani mada pana hulenga mambo mengi na hivyo huleta matatizo katika utekelezaji wakati unapofanya utafiti.

 

Isitoshe, matokeo yake pia hayashuluhishi tatizo lolote maalum kwa sababu yana ugumu wa kupima utabiti na udhaminifu wake kuambatana na vigezo vya utafiti. Vilevile, mada finyu pia haistahili (si mwafaka) kwa sabau haitakupa matokeo ya kuridhisha kwa hivyo mada nzuri ya kifanyiwa utafiti ni mada wastani. Mtafiti anaweza anza kwa kuchagua mada pana kisha aivunje hadi apate mada wastani.

 

 

 Mifano:

(a)            Athari ya dawa za kulevya nchini Kenya

(b)   Athari ya dawa za kulevya kwa wanafunzi wa chuo kikuu cha Kenyatta

(c)    Athari za dawa za kulevya katika wanafunzi wa darasa la nane chuo cha Kenyatta

 

Katika (a) Kenya ni kubwa na ina kaunti nyingi anayeiona mada hii atajiuliza ikiwa mtafiti ataweza kusanya data nchi nzima, kwa wakati ufaao pia gharama itakuwa ghali vile vile wanafunzi wa darasa la nane ni wachache matokeo hayatakuwa ya kuridhisha. (b) Ndiyo mada wastani, kwa hivyo uzingatie ikiwa mada utakayochagua itakuelekeza kuyafikia matokeo au la ikiwa jibu lako ni la

(i)                 Achilia mbali mada hiyo na utafute nyingine

(ii)               Irekebishe kwa kuifungia katika mipaka maalum itakayokusaidia kazi yako vyema.

 

Kulingana na Charlotte S. W. na Ryanga A. (2002). Unaweza kutambua mada mbaya isiyoweza kutafitika, ama kuwa na suluhisho mwafaka kwa kuzingatia vidokezo hivi:

  • Ikiwa ni pana mno na haizingatii swali maalum
  • Ikiwa inashughulikia tatizo lisilo na suluhisho linalobainika
  • Ikiwa utafiti huo hautajaza pengo lililoachwa na watafiti wengine katika uvumbuzi wao ama kuthibitisha au kukanusha kigezo kipya cha nadharia.

 

Kwa ajili ya utaratibu unaohusu utafiti, wataalamu wa utafiti Barzun na Graff (1957) walisema: kusoma, kuandika na kutafakari ni mambo matatu muhimu. Katika shughuli ya utafiti mtafiti atafakari na kuchunguza mada yake ili afahamu dhana zote zilizopo.

UUNDAJI WA SWALA LA  UTAFITI

Katika uundaji wa swala la  utafiti hatua zifuatazo huzingatiwa

(i)                              Mahitaji ya mada ya utafiti/(urgency).

(ii)                           Umuhimu wa mada hiyo kwa jumla, mada hiyo inawaathiri watu gani, kwa kiwango gani na kwa kiasi kipi?

(iii)                         Gharama na vitu vingine ambavyo vitaweza kukamilisha mada hiyo.

(iv)                         Utumikaji, mapendekezo ya utafiti yanaweza kutimika?

(v)                           Usitafiti mada zilizofanyiwa utafiti tayari.

(vi)                         Chunguza usije ukawa unamwathiri mtu yeyote katika utafiti.

(vii)                       Ni bora kutafiti kuhusu mada ambayo huungwa mkono na watu walio na mamlaka.

Hatua za Kuchagua swala la utafiti.

Kuna mambo kadha yatakayo kupatia mada ya utafiti. Yaweza kutokana na:

  • Nadharia zilizopo (existing theories)
  • Tajriba ya maisha ya jamii
  • Kadhia na harakati za maisha
  • Utafiti uliotanguliwa kufanywa (previous research studies and relications)
  • Tajriba ya mtu (personal experience)
  • Kongamano na majarida mbalimbali (discussion with experts)
  • Vitabu, tasnifu na majarida mbalimbali (books, theses and other written materials)
  • Vyombo vya habari (assertions from the media)
  • Maoni na mapendekezo ya wataalam, halmashauri ya watu wa ngazi za juu .

 

(i) Nadharia zilizopo

Nadharia ni kundi la sheria zilizopangwa katika utaratibu na mfumo maalum. Ni muhtasari wa muingiliano na uhusiono wa ujuzi wa kijumla ambao tayari upo. Husaidia kuzua jambo la kutafitiwa. Pia humuongoza mtu kwenye masuala ya utafiti ikiwa mada inayoshughulikiwa imejikita katika misingi ya kinadharia.

(ii) Kadhia na harakati  za maisha

Kila jamii ina visa mbalimbali na hali wanazokabiliana nazo kila wakati. Kama magonjwa, uhusiano, matumizi ya lugha magazetini na muingiliano wa tamaduni mbalimbali. Haya yote hudhihirika katika taathira mbalimbali. Wakati mwingine mambo haya hujadiliwa katika ngazi ya kitaifa na swala lako laweza kutokana na mambo kama haya.

 

(iii) Utafiti wa Awali

Ripoti za tafiti zilizofanywa awali huelezwa katika sura ya mapendekezo ambapo mtafiti anayetamatisha kazi yake bado anaona utafiti zaidi unahitajika. Uchunguzi zaidi ukifanywa huongeza ujuzi na ubora wa kazi hiyo. Pia mtafiti huweza kuchunguza jinsi nadharia fulani ilivyotumika na akubaliane au asikubaliane nayo kwa kuondoa utata unaoleta ubishi. Anaweza kuonyesha kuwa nadharia haikufaa katika kazi ile hivyo atachukua ripoti hii na kuifanya msingi wa suala lake la utafiti.

(iv) Tajriba ya Mtu Binafsi

Suala la utafiti linaweza kutokana na mambo ambayo mtafiti mwenyewe ameshuhudia. Mfano: mtu aliyenusurika katika mkasa wa Westgate anaweza kufanya utafiti kuhusiana na usalama au jinsi serikali ilivyotayari katika kukabiliana na vita kama hivi.

(v) Kongamano na Mijadala ya Wataalamu

Mjadala na kongamano ya wataalamu kuhusu mambo yanayotendeka kwa wakati huo na kutokana na warsha au mikutano kama hiyo, mtafiti akihudhuria huweza kupata mada ya utafiti kwa sababu wanaoshiri katika mikutano hiyo ni watu waliobobea katika nyanja hiyo.

(vi) Vitabu, tasnifu na majarida mbalimbali

Unaweza kupata suala lako la utafiti kwa kusoma vitabu vilivyoandikwa na wataalamu mbalimbali. Unaposoma unapata mwanga na kutambua suala la utafiti, kusoma zaidi ni kuelimika zaidi.

(vii) Vyombo vya Habari

Kuna mambo mengi yanayoendelea katika vyombo vya habari taarifa, mijadala na habari zinazochapishwa kila uchao, haya yote yanaweza kumwezesha mtafiti kutambua suala lake la utafiti.

(viii) Maoni na mapendekezo ya wataalamu, halimashauri na watu wa ngazi za juu

Haya ni mambo au mitazamo mbalimbali ya watu wenye ushawishi katika jamii kuhusu maswala fulani yanayohitaji kufanyiwa utafiti haswa hapa nchini Kenya. Mfano katiak idara ya usalama hapa nchini Kenya.

Vipimio vya swala la  utafiti

1.       Uhalisia, uzito na ueneaji wa mada ya utafiti

-          Ukubwa na utokeaji wa mada ya utafiti. Yaani hutokea mara kwa mara, kwa kiwango kipi? Na unathiri vipi na mathara yapi huletwa na mada hiyo ya utafiti?

2.      Nini kinachosababisha utokeaji na uendeleaji wa mada hiyo ya utafiti. Chunguza kwanza zile sababu ambazo husababisha tatizo hilo.

3.      Fafanua kwa nini wataka kufanya utafiti

4.      Elezea mkutadha ambao mada ya utafiti hutokea.

Hatua za uanishaji wa mada ya utafiti

1.       Kueleza mada ya utafiti kwa ujumla.

2.      Kuelewa uhalisia ambao unatokea.

3.      Kutembela/kurejelea makisio ya maandishi yanayopatikana.

4.      Kufafanua mada ya utafiti.

5.      Kueleza mkutadha inamotokea.

6.      Buni nadharia tete, maswali ya utafiti n.k

Sifa za Mada Nzuri ya Utafiti

Christensen L. B. (1985) (Experimental Methodology)

Anasema kuwa suala nzuri la utafiti lisilo na utata husaidia kwa kudhihirisha aina ya vifaa vya kukusanya data, aina ya data inayokidhi upimaji wa nadharia tete na mbinu mwafaka za uchunguzaji wa data. Hii ina maana kuwa mada nzuri lazima ikuongoze kwa vyovyote vile.

 

Hizi ni baadhi ya sifa za mada mwafaka

  • Ilenge tatizo maalum ambalo ndilo pengo linalofaa kushughulikiwa
  • Ikuongoze katika kupata suluhu kwa tatizo hilo na suluhu hilo liwe la kuleta faida
  • Iwe na upeo na mipaka maalum
  • Ieleweke kwa urahisi
  • Uwezekano hasa katika upeo na mipaka

 

Hivi ndivyo vigeu utakavyotumia kutambua iwapo mada yake ina upe na mipaka maalum:

  • Muda – iwe ya kutekelezwa kwa muda ufaao
  • Gharama ya utafiti
  • Vifaa utavyohitaji katika utafiti wako
  • Faida ya utafiti. Je utapata maarifa mapya, tajriba na jambo jipya litakalokujenga baada ya utafiti au la? Angalia manufaa wala sio kufanya tu kwa ajili unahitajika kufanya utafiti.
  • Ilete changamoto kwa mitazamo fulani ambayo jamii imeshikilia. Kwa mfano, nafasi ya wanawake katika jamii.
  • Ikuwezeshe na kurahisisha mbinu za kupata data yako ili utekeleze kazi yako vyema. Kwa mfano, usichague mada ambayo unajua hutapata data kwa urahisi. Mfano habari za jela, itakusumbua kupata kibali kuwahoji wafungwa.

 

3)      Maswali ya utafiti

        i.            Mugenda na Mugenda (2012:281) wanasema kwamba maswala ya utafiti yanapaswa kuwa:

(a) Dhahiri

(b) Bayana

(c) Maalum

(d) Mahususi

      ii.             Haya ni maswahili mahsusi yanayoulizwa na mtafiti kwa mujibu wa kauli ya uchunguzi ili kumsaidia na kumwelekeza katika vipengele vya utafiti.

    iii.             Huwa mafupi na bayana kwa kuwa yanatafuta majibu yatakayoleta suluhisho katika suala la utafiti. (iv) Huweka mipaka kwa kubainisha upeo wa utafiti na rasilmali zote kwa jumla.

    iv.             Kila suala la utafiti huweka wazi aina ya data inayonuiwa kukusanywa, na mbinu zinazohitajika kuifikia na kuichanganua.

Mfano

Mtafiti anataka kuchunguza kiasi, kimo, upana au kina na sababu zinazohusu dhuluma za kimapenzi miongoni mwa wafanyakazi wa sekta ya afya. Yafuatayo yatakuwa miongoni mwa maswali yanayoweza kupelelezwa:

(a) Dhuluma za kimapenzi zimeenea kwa kiasi gani miongoni mwa wafanyakazi wa kike?

(b) Sera zipi kuhusu dhuluma za kimapenzi zinapatikana katika vituo vya afya?

(c) Mafunzo katika masuala yanayohusiana na dhuluma za kimapenzi miongoni mwa wafanyakazi yanatambuliwa kwa kiasi gani?

 

4)      Malengo ya utafiti.

Malengo ya utafiti hufafanua maswala maalum ambayo utafiti kutimiza.

Sifa za malengo ya utafiti.

·         Huwa ni maelezo kamilifu ambayo yanatarajiwa kutimizwa(SMART)

·         Yawe na uhusiano wa moja kwa moja na swala la utafiti na yaweze kutafitika.

·         Yawe ya kuweza kutimika kwa wakati mahsusi au maalum.

·         Hutoa muhtasari wa yale ambayo yanakusudiwa kukamilishwa.

·         Huwa malengo maalum ambayo mtafiti angependa kutimiza.

·         Huelekeza katika kupata majibu ya utafiti lengwa kwa kuzingatia nadharia tete iliyopo.

Malengo ya utafiti hugawika katika makundi mawili:

·         Malengo wazi/jumla

·         Malengo mahsusi

Malengowazi na mahsusi si mamoja hivyo basi yasishughulikiwe kwa wakati mmoja.

Malengo wazi.(General objectives)

·         Huwa mapana mno

·         Hueleza kile ambacho mtafiti angependa kutafiti kwa kwa ujumla.

·         Huwa machache.

Malengo mahsusi(Specific objectives).

·         Ni ya muda mfupi na yana upeo mdogo sana.

·         Hupatikana tu baada ya kuvunjwa kwa malengo wazi.

·         Hupatikana kwa kutimizwa kwa malengo wazi

·         Huwa mengi mno

·         Ni lazima yaelekeze wazi mtafiti atafanya nini, wapi na kwa nini?

 

Malengo wazi hufafanua mchango wa utafiti katika uwanja mpana huku yakieleza bayana lengo la utafiti.

Malengo wazi ni malengo ambayo utafiti unakusudia kutimiza huku malengo mahsusi ni matokeo hususan ambayo hujitokeza kwa wakati teule.

Umuhimu wa malengo ya utafiti.

Malengo ya utafiti:-

·         Humwezesha na kumwelekeza mtafiti kwa kumpa mwelekeo ufaao wa kutafiti.

·         Humwezesha mtafiti kuepukana katika kukusanya data data ambayo si muhimu katika utafiti husika.

·         Kupanga utafiti wake kwa utaratibu ufaao.

·         Malengo mahususi yaliyopangwa ifaavyo huelekeza utafiti kwa kuweka mbinu ambazo zinahakikisha kuwepo kwa  Ukusanyaji, uainishaji na uchanganuzi wa data ufaao.

Madhumuni ya utafiti ni kutafuta majibu kuhusu maswali kupitia njia na taratibu za kisayansi. Lengo kuu la utafiti ni kuvumbua ukweli ambao umejificha na haujavumbuliwa na yeyote. Ingawa kila aina ya utafiti ina malengo mahsusi malengo ya utafiti yanaweza kugawika katika makundi yafuatayo:

(i)              Kuelewa swala fulani au kupata uelewa mpya. Tafiti kama hizi huitwa chunguzi (Exploratory or formulative research).

(ii)            Kudhihirisha kwa usahili zaidi sifa za mtu fulani hali fulani au kikundi fulani. Tafiti hizi huitwa tafiti elezi (descriptive).

(iii)          Kutathmini kitu fulani hutokea mara ngapi baada ya muda fulani (frequency). Tafiti hizi huitwa tafiti fumbuzi (diagnostic).

(iv)          Kutathmini nadharia tete (haipothesia) ambayo inadhihirisha uhusiano wa kisababishi baina ya vitu viwili. Tafiti hizi zinaitwa za tathmini ya ‘haipothesia’ (hypothesis – testing).

 

 

 

Marejeleo.

·         Adam, J na Kamuzora, F (2008) Research Methods for Business and Social Studies. Morogoro: Mzumbe Book Project.

·         Bowern, C (2008) Linguistic Fieldwork: A Practical Guide. New York: Palgrave-     Macmillan.

·         Kothari, C.R (2004) Research Methodology: Methods and Techniques. New Delhi: New    Age International.

·         Msokile, M (1993) Misingi ya Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: EAEP.

·         Mulokozi, M.M. (1983) “Utafiti wa Fasihi Simulizi” katika TUKI Makala ya Semina ya  Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili III: Fasihi. Dar es Salaam: TUKI.: kur. 1-25.

·         Ogechi, N.O, N.L  Shitemi, na K. I. Simala (wah) (2008) Nadharia katika Taaluma ya Kiswahili na Lugha za Kiafrika. Eldoret: Moi University Press.

·         Pons, Valdo (Mh) (1992) Introduction to Social Research. Dar es Salaam: DUP.

·         Sewangi, S.S. and Madumulla J.S. (eds) (2007) Makala ya Kongamano la Jubilei ya TUKI (Vol. I and II) Dar es Salaam: TUKI.

·         Simala, K.I. (mh) (2002) Utafiti wa Kiswahili. Eldoret: Moi University Press

 

 

 

 

No comments:

Post a Comment