KWA KUREJELEA RIWAYA YA CHOZI LA HERI, FAFANUA MAUDHUI YA
MIGOGORO YA KIJAMII.
Mgogoro ni hali ukinzani fulani ambao mhusika
anaweza kukumbana nao hasa anapoyajenga maudhui ya kazi ya fasihi. Mhusika
anaweza kuwa na mgogoro wa kindani ambao husababishwa na yeye mwenyewe kifikra
hasa anapojaribu kuyatatua maswala fulani kuhusu mazingira yake. Kwa upande
mwingine ipo migogoro inayosababishwa na
mwingiliano kati ya mhusika na wahusika wengine katika kazi ya fasihi.
Kumekuwa na ongezeko la migogoro katika jamii mbalimbali. Kumekuwa na ugomvi,
vita, talaka na hata mauaji katika jamii mbalimbali. Migogoro katika jamii zetu
husababishwa na misimamo tofauti ima ya mtu binafsi au jamii fulani kwa jumla.
Kwa hivyo migogoro ni mivutano na mikinzano mbalimbali katika kazi ya fasihi.
Wakati mwingine migogoro inaweza kuwa na
mizizi yake katika familia zilizomo katika kazi teule ya fasihi. Kila familia
huwa na misimamo na mbinu ya kipekee ya kukabiliana na maisha . Utofauti huu
ambao Waaidha uneweza kuwa unasukumizwa na mielekeo ya kibinafsi kifamilia
huleta dhana ya mgogoro huku ikizingatiwa kuwa kila jamii inaandama maisha
kivyake.
Mbali na hayo migogoro inaweza kutokea kwenye
misingi ya kitabaka. Katika msingi huu tabaka la juu hujiona kuwa bora kuliko
lile la chini huku likilikandamiza tabaka la chini. Kwa upande wake lile la
chini hujiliwaza kwa imani kuwa kila kiumbe ni bora machoni pa Muumba. Hali ya
ukinzani hudhihirika wazi hasa matabaka haya mawili yanapojikuta katika shughuli fulani ya kijamii. Hata hivyo tabaka
la juu huongozwa na kiburi na dharau dhidi ya hali duni ya tabaka la chini.
Nyadhifa mbalimbali za kikazi au madaraka,
wakati mwingine huzua hali ya mgogoro kati ya watawala na watawaliwa. Wakati
mwingine watawala huwakandamiza watawaliwa kwa kuwanyanyasa na kuwasahaulia
mbali kwa kutaka maamuzi yao pekee ndiyo bora. Hali hii inapotokea basi
ukinzani hujitokeza moja kwa moja kati ya makundi haya mawili.
Migogoro vile vile inaweza kusababishwa na
hali tofauti ya kiuchumi katika jamii zilizomo kwenye kazi ya fasihi. Pia
nafasi tofauti ambazo wahusika wanazo huwa pia hoja changizi katika makuzi ya
migogoro bila kusahau hali tofauti za misimamo ya wahusika kisiasa.
Katika
riwaya ya Chozi la Heri migogoro imejitokeza katika wahusika na viwango
mbalimbali.Migogoro hii imewaathiri wahusika binafsi pamoja na jamii nzima ya
uhusika katika kazi hii. Migogoro hii imejadiliwa kwa mapana kama ifuatavyo:-
Kuna mgogoro kwenye familia ya Mzee Mwimo
Msubili, kwa sababu familia yake ilikuwa kubwa na hakuitosheleza kwa chakula.
Uk 9,"Wingi wa vinywa vya kulishwa ulizua uhasama, migogoro na hata
uhitaji mkubwa "
Mgogoro huu uliiandama familia ya Mzee Mwimo
Msubili vikali sana. Kwanzia ukurasa wa tisa tunaona vile jamii yake inavyoana
kubanana katika vipande vidogo vidogo vya ardhi kwa kuwa ni wengi kuliko ardhi
aliyoimiliki Mzee Mwimo Msubili. Mwandishi anaichora taswira hii kwa kurejelea
hali halisi ya kimaumbile ambapo kitu chcochote kinapobinywa na kukandamizwa
hujaribu kufurukuta ili kupata nafasi ya kupumua.
Mgogoro huu ulimsababisha Mzee Mwimo
kuwatafutia wanawe Hifadhi wajinusuru na hali hiyo ngumu katika kuwahamishia
wake wawili wa mwisho kwenye Msitu wa Heri au Ughaishu kama walivyouita watu wa
huko. Hii ndiyo iliyokuwa njia ya pekee ilisalia ili kutatua hali iiyomkabili
Mzee Mwimo Msubili. Huko alikowahamishia kulikuwa afueni kwani waliweza kupata
vipande vya ardhi na kuvitumia vilivyo ili kukidhi haja zao za kucha kutwa
zikiwa ni pamoja na kupata maakuli ya kuitosheleza jamii hii.
Upo mgogoro mwingine wa kijamii unajitokeza baada ya mkoloni
kupuuza sera za Mwafrika.Uk 10,"Hatua ya mkoloni ya kupuuza sera za
Mwafrika za umiliki wa ardhi na kuamua kujumuisha pamoja ardhi iliyomilikiwa na
mtu binafsi na kuuidhinisha umiliki huu kwa hatimiliki, ilivuruga mshikamano wa
kijamii "Kwa yakini wakati wa uvamizi wa mataifa yanayoendelea na mkoloni,
hali ambayo haikusazwa ni ile ya kuyanyakua mashamba ya wakazi asilia huku
wakoloni wakijilimbikizia mashamba pasi kujali athari hizo kwa wenyeji. Mkoloni
alifanya hivi kwa kupuuza sera za Mwafrika za kumiliki ardhi na kuamua
kujumuisha pamoja ardhi iliyomilikiwa na mtu binafsi, na kuidhinisha kijamii.
Katika sera ya kijadi ya umiliki na matumizi ya ardhi, raia wote, hata wageni,
walikaribishwa na kugawiwa mashamba, hivyo kupata mbinu za kujiendeleza
kimaisha.
Mgogoro ulizua utata baina ya jamii asilia na
zile za wakoloni kwani uhasama uliokithiri na kukolea akilini mwa waja. Wale
walioyamiliki mashamba kabla ya kuja kwa wakoloni, waliohisi kuwa ukoloni
umewavamia na kuteka nyaya rasilmali yao ya ardhi. Hali hii ilisababisha chuki
baina ya waathiri na waathiriwa kwa kuwa urasmi wa umiliki wa ardhi yao
uliwatoweka na kunaswa na wakoloni ambao licha ya kuwanyang’anya ardhi yao waliwafanya watumwa.
Kwa upande wa wenyeji, kulizuka hali ya
uhasama kwa kuona kuwa wale Waliokosa mahali pa kujisitiri wakajiona kama
wasiofaa katu. Wengine hasa waliopoteza mashamba yao na kulazimishwa kuyafanya
ya kitaifa. Mgogoro huu ulisababisha uhasama ambao kuondoa si rahisi na pia
mgogoro kama huu, huhamisha na kuathiri ujumla wa waathiriwa na jamii kwa jumla
katika nyanja mbalimbali.
Kulijitokeza mgogoro shuleni wakati Ridhaa
aliitwa 'mfuata mvua',na kutengwa na wenzake. Uk 10,"Wewe ni mfuata mvua.
Hatutaki kucheza nawe. Umekuja hapa kutushinda katika mitihani yote. Wewe ndiwe
unayetuibia kalamu zetu "Walimwona kama mwizi. Ridhaa alikuwa mojawapo wa
waathiriwa na ubaguzi akiwa shuleni.Aliweza kutengwa na wenzake hasa walipokuwa
wakichaeza mchezo wao wa Kavuta ambao
unachezwa na kupendwa sana na watoto wa kusukuma Vifuniko vya chupa za soda kwa
ncha za vidole vyao. Hali hii ilimwathiri sana Ridhaa na hata alipofika
nyumbani kwao akajitupa sakafuni na kulia kwa kite na shake. Mama yake
alipowasili hakusita ila kupendekeza asirudi shuleni kwa kuhofia kuchekwa na
wenzake kila mara.
Hata hivyo mama mtu anampa wosia kuwa asiwe
mtu wa kutoka tamaa kwa haraka hasa akiwa shuleni.Shule ama elimu aione kama chombo cha kueneza amani na upendo
wala sio fujo na chuki. Alizidi kumshauri kuwa huenda mwenzake alikuwa na hofu kwa
vile alionao uhuru wake umeingiliwa. Na kutokana na ushauri huo, Ridhaa akapata
mwanzo wa maisha ya heri.uk.11.
Ridha kibinafsi anajikuta katika mgogoro
katika nafsi yake mwenyewe. Uk 12,"Miguu yake sasa ilianza kulalamika pole
pole parafujo za mwili wake zililegea, akaketi juu ya ya wapenzi wake. Baada ya
muda wa mvutano, wa hisla na mawazo, usingizi ulimwiba. Hii ilitokana na
kugundua kuwa mahali alipoishi hapakuwa pake haswa tangia mwanzoni. Hii
ilitokana na dalili za vitushi ambavyo vilimwandama. Anajaribu kupiga taswira
nyuma kuhusu namna alivyokuja kumiliki kipande cha ardhi alichokijengea nyumba
yake kwa kuuziwa na dadake Kendi sehemu hiyo ikiwa msitu.
Alitia juhudi kuhakikisha kijiji kizima
kinapata maji safi ya mabomba ambayp maji haya yaliweza kubadili mazingira ya
pale yaliyokuwa sawa na jangwa la Kalahari hadi kuwa ardhi ya chanikiwiti yenye
rutuba si haba. Maswali chungu nzima yalimwandama akilini akakose majibu.
Hakujua apige ukemi au afanyeje. Akiwa katika
hali hiyo ya mgogoro wa kinafsia, ndipo anaanza kukumbuka na kuelewa mambo mbalimbali yaliyokuwa yakitendeka kama
kusambazwa kwa vikaratasi vikiwatahadharisha kuwa kulikuwepo na gharika mbeleni
baada ya kutawazwa kwa Musumbi(Kiongozi) mpya, kukatwa kwake mguu na jirani
yake mara moja pamoja na ile hali ya mke wa jirani yake kulalamikia kuuzwa kwa
shamba la wenyeji kwa wageni.
Kulikuwa na mgogoro uliosababishwa na
wanasiasa, juu y nani atakaye kuwa kiongozi wa jamii, kati ya mwanamke
mwananume. Uk 19,"MijadaIa hii ilizua na kukuza migogoro isiyomithilika
". Kuhusu hali hiyo mgogoro huu uliathiri hali mbalimbali za eneo hilo.
Kila kikundi kilikuwa kikiunga mkono msimamo wao.
Matokeo yake yalikuwa pamoja na kutenda kwa
hali ya taharuki ilitanda ambapo vyombo vya madola vikatumwa kudumisha Usalama
katika vijiji, mitaa nayo ikajaa polisi wa kuzima vurugu katika kila pembe.
Kuwepo kwa vikosi vya polisi katika mitaa ya watu hakukusaidia chochote bali
kulizidisha migogoro baina ya pande hizo mbili hasimu. Kila upande uliona kuwa
huenda ikawa walienda Usalama walikuwa na nia ya kuwaondoa viongozi
waliowapigia debe madarakani.
Baada ya kura wagombezi wote walijikalia
majumbani mwao na kuwatazama kwenye
runinga namna Wafuasi wao walivyozozana. Katika hali hii mchezo wa pata shika
polisi kukimbizana na raia huwa jambo la kawaida. Ikumbukwe kuwa raia huwa
hawana silaha hatari kama walizo nazo polisi hivyo basi hii hupelekea kuuawa
kwa watu wasio na hatia kiholela huku polisi wakinadi kuwa wanatuliza vurugu.
Mgogoro mwingine ulijitokeza kati ya raia na
wanapolisi, wakiwa katika harakati zao za kuweka amani. Uk 19,"Mchezo wa
polisi kukimbizana na raia ulianza katika mchezo huo mamia ya roho zisizo na
hatia zilisalimu amri chini ya pambaja za risasi na mapigo ya rungu, vitoa
machozi navyo vikafanya kazi barabara. Hii ilitokana na hali ya kuweka usalama
baina ya wafuasi wa wagombezi hao. Hii husababisha polisi kujipata kwenye
mgogoro mkubwa na raia wasio na hatia.
Walinda usalama huajaribu kwa jino na ukucha
kutumia mbinu zozote zile mradi zitawasaidia kukomesha vurugu baina ya Wafuasi
ingawa Wafuasi hawa nao huwaona polisi kama adui wao mkubwa ambaye ana nia ya
kuwazuia kutekeleza katiba yao kama demokrasia ya nchi inavyonadi.
g)Nyamvula anajikuta katika mgogoro wa nafsi
yake, wakati ambapo imani yake inakinzana na kazi ya kuwa askari. Uk
62,"Kulingana na Nyamvula, kuwa askari wa vita kulikinzana na imani yake,
hasa kwa vile Nyamvula alisema ni born again. Mwangeka alimsisitizia kuwa
kulinda usalama si sawa na kuua " Hapa Nyamvula anajikuta katika njia
panda asijue la kufanya hasa baada ya rafiki yake kumithilisha kazi ya ulingaji
usalama na dhambi ikichukuliwa kuwa Nyamvula ni mwokovu.
Katika
ukurasa wa 38 Tila anaitaja migogoro kadha iljYO katika Tamthilia ya Hussein.
Tamthilia hii ya Mashetani ninayorejelewa ina migogoro mingi sana kama:
migogoro ya kisiasa, kiuchumi, na pia ya kijamii.
"Tila:
Nadhani
umesahau baba. Suala hili ulisema limeshUghulikiwa katika kazi za kifasihi kama
vile Mashetani, ile tarnthilia ya Hussein inayoisawiri migogoro ya kisiasa,
kiuchumi na kijamii ya baada ya ukoloni lsitoshe, mwalimu alitaka tu kuonyesha kwamba upo uhusiano kati ya mfumo wa kiuchumi
na mfumo wa kisiasa alituambia kwamba mfumo wa kiuchumi hudhibitiana na mfumo
wa kisiasa. Utawala huteuliwa makusudi kuendeleza mfumo uliopo wa kiuchumi kwa
maslahi ya watawala na tabaka ambalo linazimiliki nyenzo za uzalishaji mali
"
Mbali
na aina hii ya migogoro, pia kuna ile migogoro inayoletwa na tofauti katika
hadhi za maisha ambapo kuna walaheri na walalahoi. Katika kazi hii ulalahoi
unadhihirika katika wahusika kadhaa. Tunapata kuwa waafrika wanajikuta katika
hali ya umasikini; Uk 7,"Waafrika waliobahatika kuwa na makao yao binafsi
walipata sehemu ambazo hazingeweza kutoa mazao yenyewe; na bila shaka hali yao
iliweza kutabirika; kuvyazwa kwa tabaka la wakulima wdogowadogo, maskini, wasio
na ardhi "
Uk
25,"Nyinyi ndio vikaragosi wanaotumiwa na wasaliti wa nia zetu kuendelea
kutudidimiza kwenye lindi hili la ukata "
Ridhaa
pia anajikuta kwenye lindi la umaskini baada ya mali yake yote kuchomwa,
ikiwemo familia yake.
Uk
1,"Ridhaa alisimama kwa maumivu makali, mikono kairudisha nyuma ya mgongo
wake uliopinda kwa uchungu. Macho yake yaliyotanda ukungu alikuwa kayatunga juu angani, akitazama wingu
la moshi lililojikokota kwa Kedi na mbwembwe; wingu lililomwonyesha na
kumkumbusha ukiwa aliozaliwa nao na ambao alihofia kuwa angeishi na kuzikwa nao.
"
Tunapata
pia kuwa watu wengi wanaiaga dunia wakijaribu kujikomboa kutokana na hali hii ya
ukata, wanapoenda kuchota mafuta kwenye lori ambalo limebingirika kisa na maana
alienda kuwaokoa watu ambao wa likuwa wakipora mafuta kutoka kwenye lori,
ambalo lilikuwa limebingiria lnasemekana kuwa umaskini uliwasukuma watu hawa
kuchukua kisichokuwa haki yao!"
Hii
ni kuwa hali hizi mbili tofauti zina ukinzani mkubwa ambao huzua migogogro kati
ya wahuka wanaopatikana katika kila pende.
Swala
la ushirikina pia limezua mgogoro wa imani kati ya jamii na kuchukuliwa kuwa
mojawapo wa nguzo zao za kimaisha. Hata hivyo, wasio na imani kama hiyo
hujikuta katika mrengo pinzani ambao huleta mgogoro katika jamii husika.
Ridhaa
anaposikia milio ya bundi, anaamini kuwa milio hii ina maana iliyofichika. Uk
1,"Anakumbuka mlio wa kereng'ende na bundi usiku wa kuamkia siku hii ya
kiyama. Milio hii ndiyo iliyomtia kiwewe zaidi kwani bundi hawakuwa wageni wa
kikaida katika janibu hizi " Uk 2,"Ninashangaa ni vipi daktari mzima
hapo ulipo unajishughulisha na mambo ya ushirikina.
Swala la migogoro pia halikusaza
familia mbalimbali katika kazi hii.Mwangeka alikutana na
Lily Nyamvula katika Chuo kikuu na kumwoa. Walibarikiwa na mtoto mmoja kwa jina
Becky.
Ndoa
hii haikudumu kwani Lily na Becky waliangamia kwenye janga la moto.Baada ya
ndoa ya mwanzo kusambaratika, Mwangeka alimwoa Apondi. Walibarikiwa na mwana wa
kiume kwa jina Ridhaa.
Mwangemi
alimwoa mwanamke kwa jina Neema. Hawakufaulu kupata mwana wao kindakindaki japo
walipanga mwana wao kwa jina Mwaliko. Hii ilisababisha migogoro katika jamii
hii kwa kukosa kufahamu chanzo chao cha kutofanikiwa kupata mtoto.
Lucia
Kiriri —Kangata-,-alikuwa ameolewa katika ukoo wa Waombwe ambao awali walikuwa
maadui sugu wa ukoo wa Anyamvua. Ndoa hii ilipata pingamizi sana kutoka kwa
ukoo mzima lakini kutokana na Msimamo imara wa Kangata ndoa hii ilisimama. Watu
wa ukoo wa kina Kangata walishangaa ni kwa nini mwana wao akaozwa kwa watu
ambao huvaa nguo ndani nje na pia huzaa majoka ya mdimu ambayo ni machoyo
kupindukia.
Lunga
alikuwa na mke kwa jina Naomi. Walikuwa na wana watatu, Umu, Dick na Mwaliko.
Ndoa hii haikudumu kwaniNaomi alimwacha Lunga na kwenda mjini alikokuwa
shangingi kwelikweli. Hii ilikuwa kwa sababu za migogoro ya mara kwa mara nasfi
ya Naomi ya kutaka uhuru wa kushiriki anasa atakavyo pamoja na kukataa kutii
kama mke katika ndoa yake.
Pete
na Fungo- tunaelezwa kuwa Pete alipoingia darasa Ia saba alipashwa tohara nao
wajombake wakapokea posa na baadaye mahari kutoka kwa buda mmoja kwa jina Fungo
aliyemuoa kama bibi wa nne. Ndoa hii haikudumu kutokana na kutoaminiana kati
ya wanandoa hawa na mwishowetunajuzwa
kuwa kwani Pete alihiari kumwacha baba
huyu kwa kuwa alionao si makamo yake katu.
Suala la ukoloni
nalo pia limechangia pakubwa kuwepo kwa migogoro katika kazi hii. Ukoloni mamboleo ni zao la uongozi mbaya. Viongozi
waanzilishi wa mataifa yaliyopata uhuru hawakuzua sera na mikakati mwafaka ya
kuhakikisha nchi zao zimepata kujisimamia kiuchumi.Misimamo hii inaleta
mafarakano katika jamii husika kama inavyojitokeza katika kazi hii.
Katika
Chozi la Heri, Waafrika wenyewe wanajifanya wakoloni juu ya waafrika wenzao,
ambao wako chini yao kitabaka au kisiasa kwa mfano katika ukurasa wa 5,mashamba
ya Waafrika yananyakuliwa na watu binafsi baada ya wakoloni kwenda, nao
waafrika wanawekwa mahali pamoja ili kuishi katika hali ya ujamaa "Lakini
baba, wewe siwe uliyeniambia kuwa mashamba ya Theluji nyeusi yalikuwa milki ya
wakoloni?na sasa yanamilikiwa na nani? Si mwana wa yule mlowezi maarufu ambaye
wewe hunitajia kila mara? Maekari kwa maekari ya mashamba katika eneo Ia kisiwa
bora yanamilikiwa na nani? Si yule myunani aliyewageuza wenyeji kuwa maskwota
katika vitovu vya usuli wao?"
Katika
ukurasa wa 24 tunapata kuwa vijana wanakufa kwa mitutu ya bunduki wanapojaribu
kujikomboa kutokana na ukoloni wa Mwafrika. Walipigania uhuru wa tatu, ambao ni
ukombozi kutokana na uongozi wa Mwafrika "Baada ya muda mfupi, vifua vyao
vilikabiliana na risasi zilizorashiwa vifua hivyo kama marashi, vifua vikawa
havina uwezo dhidi ya Shaba, vijana wakaanguka mmoja baada ya mwingine,
wamekufa kifo cha kishujaa, wamejitolea mhanga kupigania uhuru wa tatu"
Vile
vile ukoloni mkongwe nao pia una mchango mkubwa katika kuwepo kwa migogogro
katika kazi hii.Huu ni ukoloni uliokuwa wa Waingereza, kabla ya nchi za Afrika kupata uhuru.
Tunapata
kuwa mkoloni anapata fursa ya kuendeleza kilimo katika sehemu za mashamba ya
Waafrika zilizotoa mazao mengi. Uk 7, "Mustakabali wa ukuaji wetu kiuchumi
uligonga mwamba wakati sheria ya mkoloni ilipompa mzungu kibali cha kumiliki
mashamba katika sehemu zilizotoa mazao mengi. Ukengeushi wa ardhi ukatiliwa
muhuri, umilikajia wa ardhi na Mwafrika katika sehemu hizi ukapigwa marufuku;
si mashamba ya chai, si ya kahawa yote yakapata wenyeji wageni dau la mwafrika
likagonga jabali.Hali kama hii inazua migogoro katika ya wakoloni na wenyeji
asilia wa eneo linaliathirika.
Katika
ukurasa wa 7 tunasoma; "Waafrika waliobahatika kuwa na makao yao binafsi
walipata sehemu ambazo hazingeweza kutoa mazao yenyewe; na bila shaka hali yao
iliweza kutabirika; kuvyazwa kwa tabaka la wakulima wadogowadogo, maskini,
wasio na ardhi. Nadhani unaweza kukisia hali ilivyokuwa kwa familia nyingi za
kiafrika. Kama vile baba
Msumbili
alivyokuwa akisema, jamii yetu iligeuka kuwa hazina kuu ya wafanyakazi ambamo
wazungu wangeamUa kuchukua vubarua kupalilia mazao yao"
Tunaona
kuwa wazungu bado waliwatumia waafrika kama wafanyakazi mashambani
'mwao',ambayo walinyakL kutoka kwa waafrika.
Ipo vile vile migogoro inayozaliwa
kwenye misingi ya kifeministi ambapo mwanamke anakosa kutambulika kama kiembe
kilicho imara na chenye usemi katika jamii. Pasi jinsia zote mbili kutambulika
migogoro katika jamii husika hudumu mile daima.
Katika
ukurasa wa 16 tunasoma; "Siku ile baada ya kutawazwa kwa kiongozi mpya,
kiongozi ambaye kulingana na desturi za humu mwetu, hakustahili kuiongoza jamii
ya wahafidhi na, kisa na maana, alikuwa mwanamke.
Katika
ukurasa wa 3;"Huku ni kujiumbua hasa. Unyonge haukuumbiwa majimbi;
ulitunukiwa makoo.”Bibi
alikuwa akimwelezea Ridhaa kuwa unyonge haukuumbiwa 'majjmbi'ambao ni wanaume,
bali uliumbiwa 'makoo',yaani wanawake. Hivyo basi tunapata kuona kuwa jamii pia
iliwadhalilisha wanawake tangu zamani.
Katika
ukurasa wa 8; "Mzee mwenye wake na wana wengi alihesabiwa kuwa mkwasi
kwelikweli basi wake hawa hawakuchelea kutimiza amri ya
maumbile,
wakapania kuujaza ulimwengu " Tunapata kuwa wanawake wanadhalilishwa kwa
kuonekana kana kwamba jukumu lao kuu katka jamii ni kuijaza dunia au kuzaa
wana. Mwanamke hapewi nyadhifa za umuhimu katika jamii ila tu kazi yake ni
kuoleka na kujaaliwa na wana wengi awezavyo.
Katika
ukurasa wa 45;"Viongozi wengi wa awali walibwagwa chini na vijana
chipukizi. La kuhuzunisha ni kwamba wengi walishindwa kabisa kukubali ushinde,
hasa yule ambaye alikuwa anagombea kilele cha uongozi. Kulingana naye, nafasi
hii iliumbiwa mwanamume, na kupewa mwanamke ni maonevu yasiyovumilika
"Katika hali hii, jamii haikukubali wanawake kuwa viongozi, bali cheo hiki
cha uongozi kilikuwa cha jinsia ya uwsanaume.
Katika
ukurasa wa 149; "Maisha yangu na Fugo yalikuwa kama ya ng' ombe aliyetiwa
shemere na kufungwa nira pamoja na punda ambaye anakaidi kusonga. UIe unene
wake, lile kituzi lililotoka kwenye makwapa yake makuza na kUfudikiza kote
chumbani, ule wivu wa mke mwenzangu wa
pili,
kule kukemewa na kuchekwa na watoto wa mke wa kwanza yote yalininyong' onyeza
na kuniumbua. Nilichukia jaala aliyonipa mama kwa kujali maslahi yake tu,
nilichukia nguvu ya maumbile iliyoniweka kwenye jinsia ya kike, nilichukia
kitoto nilichohimili kwenye mji wangu hata miezi tisa ilipotimia na kupata
salama, niliamua kwamba kwa mzee Fungo hakuniweki tena.
Na
unadhani anakwenda wapi?Utawezaje kujitunza wewe na mtoto wako na hali bibi
yako ndiye huyohana hanani, na wazazi wako walafi walikuuza kwangu ili wapate
pesa za kuwasomesha ndugu wako watano wa kiume?AliulizaFungo "Tukio hili
linatuonyesha wazi jinsi mwanamke amedhalilishwa katika jamii. Hivyo basi jamii
haikosi kuwa na migogoro hadi hapo mwanamke atakapopewa nafasi yake.
Kwanza,
mamake mtoto huyu msichana anamwoza kwa mzee mwenye wake wawili, (Mzee
Fungo),ili aweze kupata pesa za kuwalipia vijana wake karo ya shule.
Msichana
anaonekana kutokuwa na umuhimu ya kupelekwa shuleni ili kupata elimu, ilhali
yeye mwenyewe aliazimia kuendeleza masomo yake. Maazimio yake ya elimu
yanagonga mwamba baada ya kuozwa ka mzee Fungo ambaye anamtesa na mwishowe
kumtaliki na kitoto kichanga.
Msicha
na huyu mchanga pia anapitia machungu kwenye ndoa yake kwa kuchekwa na
kudharauliwa na wake wenzake na wana wao.
Hitimisho.
Migogoro huweza kuwa kati ya wahusika ambapo
wahusika hawa huwa na misimamo inayotofautiana kabisa kuhusu hali tofauti za
kimaisha. Mgogoro kama huu huonekana kana kwamba umeipiku migororo mingine
yoyote ile kwa kuwa matukio yote katika kazi yoyote ya fasihi huendeshwa na
kuelekezwa kupitia viumbe hawa. kwa kuwa suala la migogoro
limekuwa tatizo sugu katika jamii zetu, ipo haja ya kujaribu kwa vyovyote kuona kuwa jambo hili linapata tiba ya
kudumu.
Marejeleo.
a.
Bouchier D. The Feminist
Challenge. London: Macmillan Press, 1983.
b.
Burleson B, Denten W. The
Relationship between Communication Skills and Marital Satisfaction: Some
Moderating Effects. Journal of Marriage and Family,1997; 59(4).
c.
Chapman G. Desperate
Marriage. Moving towards Hope and Healing in Your Relationship. Chicago:
Northfield Publishing, 2008.
d.
Mugenda O, Mugenda A. Research
Methods: Quantitative and Qualitative Approaches. Nairobi: Acts Press,
1999.Ogechi N. Mbinu za Mawasiliano. Eldoret: MoiUniversity Press, 2002.
e.
Wamitila K. Uhakiki
wa Fasihi, Misingi na Vipengele Vyake. Nairobi: Phoenix Publishers Ltd,
2002.
f.
Republic of Kenya The
Constitution of Kenya, 2010: Kenya Gazette Supplement. Nairobi: The
Government Printers, 2010.
g.
Assumpta, K.H(2014). Chozi
la Heri, One planet Publishing & Media services Limited, Nairobi.
h.
TUKI, (2004) Kamusi ya
Kiswahili Sanifu. Oxford University Press: Nairobi.
i.
TUKI (1990) Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha . Dar es Salaam, University of Dares Salaam.
j. Wafula, R.M.& Kimani Njogu (2007). Nadharia za Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.
k. Wafula, R.M. (1999). Uhakiki wa Tamthilia: Historia na
Maendeleo Yake. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.
l. Wamitila, K.W. (2003). Kamusi ya Fasihi: Istilahi na Nadharia. Nairobi: Focus Books.
m. Wamitila, K.W. (2002).
Uhakiki wa Fasihi.
Nairobi: Phoenix.