Monday

mchango wa fasihi iliyotafsiriwa katika fasihi simulizi

0 comments

 

FAFANUA MCHANGO WA FASIHI ILIYOTAFSIRIWA JUU YA FASIHI SIMULIZI....

Utangulizi

Kwa muda sasa, kumekuwepo na ongezeko kubwa la kazi za Kiswahili zilizotafsiriwa kutoka katika lugha zingine mbalimbali. Ongezeko hili limechangia pakubwa katika kuwepo kwa kazi nyingi za fasihi ya Kiswahili ikiwemo fasihi simulizi. Tamthilia, riwaya, hadithi fupi, mashairi, pamoja na tanzu mbalimbali za fasihi simulizi na hata tungo zingine katika lugha za kigeni na za kiafrika sasa zinaweza kusomwa katika lugha ya Kiswahili. Mchango huu mkubwa bado haujatambuliwa na wasomi wengi ambao miongoni mwao ni wale wanaofaidika na tafsiri hizi.

Tafsiri hizi hata hivyo zimeandamwa na changamoto chungu nzima katika kuhakikisha kuwa tunapata tafsiri faafu za kazi za lugha ya kigeni. Hivyo basi, kazi hii inalenga kudadisi mchango wa kazi zilizotafsiriwa katika kuendeleza lugha na fasihi ya Kiswahili pamoja na kuchanganua changamoto zinazoambatana na tafsiri za kazi hizi. Aidha, makala haya yanalenga kuonyesha umuhimu wa kudhamini kazi hizi, kuzichunguza upya tena kwa nia ya kuzikosoa na zaidi ya yote kupendekeza njia mwafaka za kuibuka na tafsiri faafu katika karne hii ya teknolojia na utandawazi.

Maana ya tafsiri

Kulingana na Larson (1994), tafsiri ni neno linalotumiwa kumaanisha harakati ambapo maana ya maelezo katika lugha moja ambayo ni lugha chasili inabadilishwa hadi maana ya lugha nyingine ambayo ni lugha lengwa. Pia, Newmark (1988), anasema kuwa kutafsiri ni kitendo cha kubadilisha kauli au habari iliyoandikwa kwa lugha moja hadi lugha nyingine.

Tafsiri hufanywa kwa lengo la kutaka ujumbe fulani ulio katika lugha isiyoeleweka kueleweka na wasomi. Crystal (1987), anasisitiza kauli hii kwa kusema kuwa watu wanapokabiliwa na lugha wasiyoielewa, humwendea mtafsiri ili waweze kufasiri habari hizo. Hii ni kumaanisha kuwa kitendo cha kutafsiri hutatua shida za kutoeleweka kwa ujumbe katika lugha iwayo yoyote. Mtafsiri huhitajika kuonyesha ulinganifu, mshikamano na pia usambamba kati ya lugha zote mbili anapofanya tafsiri.

Tafsiri ni taaluma ambayo imeshughulikiwa kwa muda mrefu na wataalamu mbalimbali. Mbali na fasihi, taaluma hii imehusisha nyanja zingine za kitaaluma kama vile isimu, filosofia, na hata mawasiliano, (Munday (2001).

Kwa upande wa tafsiri, Catford akinukuliwa na Mwansoko (2006) anasema tafsiri ni kuchukua mawazo yaliyo katika maandishi kutoka lugha moja (lugha chanzi) na kuweka badala yake mawazo yanayolingana katika lugha nyingine (lugha lengwa).

Naye Newmark (1982) anaeleza kuwa tafsiri ni mchakato wa uhawilishaji wa maneno kutoka matini chanzi kwenda matini lengwa.

Pia Nida na Taber (1969) wanaeleza kuwa tafsiri hujumuisha kuzalisha upya ujumbe wa lugha chanzi kwa kutumia visawe vya asili vya lugha lengwa vinavyo karibiana zaidi na lugha chanzi kimaana na kimtindo. Wao wanatilia mkazo uzalishaji upya wa kwa kutumia visawe asili vinavyokaribiana na matini chanzi kimaana na kimtindo. Kutokana na maana hizi tunaweza kusema kuwa tafsiri hufanywa katika ujumbe uliopo katika maandishi, ni jaribio la kiuhawilishaji na wazo linalatafsiriwa huwa na visawe vinavyokaribiana na sio sawa kutokana na tofauti za kiisimu, kihistoria, kiutamaduni na mazingira.

Kwa ujumla tafsiri ni mchakato wa uhawilishaji wa mawazo, ujumbe au maana katika maandishi kutoka lugha moja hadi nyingine (kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa).

Kwa hivyo, tafsiri ni taaluma ya uhawilishaji wa mawazo katika maandishi kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa kwa kuzingatia isimu, mukutadha na utamaduni. Taaluma ya tafsiri imeanza hivi karibuni mara baada ya majilio ya maandishi. Hii ina maana kwamba baada ya kuwepo kwa maandishi ndipo taaluma hii ya tafsiri ikaanza.

Taaluma hii ya tafsiri huhusisha stadi kuu nne za muhimu ambazo ni kusoma, kuandika, kusikiliza na kuzungumza. Mfasiri anatakiwa kuwa na ujuzi wa taaluma hii ili kufanikisha mchakato wa tafsiri kwa ufanisi.

Mchango wa kazi zilizotafsiriwa katika uga wa fasihi andishi na simulizi.

Taaluma hii imeendelea kukua kadiri muda unavyosonga. Kwanza kabisa, tafsiri imechangia kuwepo kwa ongezeko kubwa la kazi za Kiswahili zilizotafsiriwa kutoka katika lugha zingine.. Ongezeko hili limechangia kuwepo kwa kazi nyingi za fasihi ya Kiswahili. Tamthilia, riwaya, hadithi fupi, mashairi na hata tungo zingine katika lugha za kigeni na za kiafrika sasa zinaweza kusomwa katika lugha ya Kiswahili. Yaani imeweza kuitajirisha fasihi ya Kiswahili. Vitabu vingi vya lugha ya kigeni hasa ya Kingereza vimetafsiriwa kwa Kiswahili na hivyo kupigisha hatua fasihi ya Kiswahili. Baadhi ya kazi hizi ni kama vile: The Well of Giningi - Kisima cha Giningi, Maisha Yangu “Moya Zhizn”, riwaya ya Andrei Zhukov 1968 Kiswahili-Kirusi, I will marry when I want - Nitaolewa Nikipenda, The Beautiful Ones are Not yet Born - Wema Hawajazaliwa, The Taste of Heaven - Aliyeonja Pepo Tamthilia, The Government Inspector - Mkaguzi Mkuu wa Serikali Tamthilia Christon Mwakasaka 1979 Kiingereza-Kiswahili, Anthology of Swahili Poetry - Kusanyiko la Mashairi, The Black Hermit - Mtawa Mweusi , Song of Lawino - Wimbo wa Lawino miongoni mwa kazi nyingi maarufu.

Kazi hizi ambazo zimetafsiriwa katika mfumo wa fasihi andishi ndizo zizo hizo ambazo zinatimiza mahitaji ya fasihi simulizi kwani hali ni ile ile isipokuwa njia ya uwasilishaji. 

Ifahamike kuwa kazi hizi sasa zinasomeka kwa Kiswahili. Ni malighafi ya fasihi ya Kiswahili kutokana na mchango wa tafsiri.

 

Kutokana na tathmini ya kina, imedhihirika kuwa tafsiri hizi za kazi ya fasihi zimefanywa sana katika kitengo cha tamthilia kuliko riwaya, hadithi fupi na Mashairi. Mwansoko (2006:46) anaeleza kuwa tamthilia ni utanzu uliotafsiriwa sana kutokana na malengo makuu mawili; lengo la kuigizwa na lengo la kusomwa. Pia umefasiriwa sana kutokana na kwamba, ulikuwa ni utanzu mpya katika Afrika, hivyo wageni na wenyeji walitafsiri kwa lengo la kuutambulisha katika mazingira ya kiafrika. Vilevile umeonekana kutafsiriwa sana kutokana na urahisi wa lugha yake, kwani tamthilia hutumia maneno machache na yanayoeleweka tena bila hata ya ufafanuzi wa kina kama ilivyo katika riwaya. Zaidi ya yote, umefasiriwa sana kutokana na umuhimu wa maudhui yake ambayo hujibainisha katika masuala mtambuko duniani kote. Kwa mfano; tamthilia ya “Nitaolewa Nikipenda na Mtawa Mweusi” maudhui yake yanahalisika katika jamii mbalimbali. Vilevile umetafsiriwa sana kwa lengo la kukuza na kueneza lugha adhimu ya Kiswahili, ambayo haikuwa na machapisho mengi yahusuyo fasihi andishi. Kwa upande wa lugha zilizojitokeza zaidi katika kufanikisha suala la tafsiri ya fasihi ya Kiswahili ni lugha ya kiingereza, na Kiswahili; lugha ya Kiingeza imejitokeza sana katika tafsiri kutokana na kwamba, waingereza ni moja kati ya mataifa yaliyotawala sehemu kubwa ya dunia, na ndio taifa lililokuwa na dola yenye nguvu zaidi. Vilevile Waingereza walishapiga hatua kubwa katika maendeleo ya fasihi ima andishi au simulizi ukilinganisha na mataifa mengine. Pia hata lugha ya Kiingereza ni moja kati ya lugha kubwa duniani na inayofahamika na mataifa mengi. Lugha ya Kiswahili nayo imeonekana kutafsiriwa sana kutokana na hitaji la kuwa na machapisho mengi ya kifasihi ili kukuza na kueneza fasihi ya Kiswahili. Pia ni lugha inayokua kwa kasi na inayoeleweka sana Afrika Mashariki ukilinganisha na lugha nyingine.

Pili, imewezesha ulinganisho wa utamaduni wa Kiswahili na ule wa kigeni. Tafsri hutusaidia kujua na kulinganisha tamaduni za jamii nyingine na ile iliyoandikiwa tafsiri. Tamthilia ya “Nitaolewa Nikipenda” imetungwa katika mazingira ya jamii ya kikuyu, hivyo tafsiri ya tamthilia hii imesaidia kujua utamaduni wa Wakikuyu. Kwa mfano katika ukurasa wa 65, tunaweza kuona jinsi ndoa ya kikuyu inavyofungwa, utaratibu wa utoaji mahari pamoja na nyimbo ziimbwazo wakatika wa sherehe. Ni muhimu kutaja kuwa kipengele cha utamaduni huwaathiri pakubwa tafsiri. Kulingana na Teilanyo (2007:16) utamaduni ni chanzo cha utata katika kutafsiri anaposema kuwa “ugumu hutokana na shida ya kupata neno mwafaka katika lugha lengwa kwa kuzingatia utamaduni wa dhana hiyo kwa lugha chasili, matokeo ya kweli ni kuwa lugha mbili huwa na maana tofauti kidesturi na kitamaduni.”

Kuna misingi miwili ya kuhakiki kazi yoyote ya tafsiri. Msingi wa kwanza ni uelewa au ujuzi. Tafsiri inatakiwa ionyeshe uelewa na ujuzi wa tamaduni tofauti. Msingi wa pili ni `sababu` au lengo la mtunzi asilia ambalo linafaa kudhihirika katika matini lengwa. Nahau, sawia na semi, hubuniwa kutokana na itikadi, mila, desturi na mazingira ya watumizi wa lugha husika. Kipengele hiki cha utamaduni huwa muhimu sana katika tafsiri. Hii ina maana kuwa nahau katika matini chasili zinapotafsiriwa sharti mtafsiri azingatie utamaduni wa lugha lengwa. Yaani, utamaduni wa lugha chasili na lugha pokezi huzingatiwa. Hii ni kutokana na sababu kwamba lugha chasili na lugha pokezi zina tamaduni zao za kipekee na ambazo zinatofautiana kwa kiwango kikubwa mno.

Imechangia kuwepo kwa tanzu mpya na za kigeni katika fasihi ya Kiswahili. Awali Waafrika waliidhamini sana fasihi simulizi. Hii ndiyo iliyokuwa fasihi yao. Hata hivyo, tafsiri imesaidia kuingiza utanzu mpya katika fasihi andishi ya Kiswahili, kwani historia ya fasihi barani Afrika inaonesha kwamba, hapo awali jamii za kiafrika hazikuwa na utanzu huu wa fasihi. Hivyo basi, kupitia tafsiri fasihi ya Kiswahili imeweza kujitanua zaidi.

Isitoshe, tafsiri imesaidia kukuza na kusambaza fasihi ya Kiswahili ulimwenguni. Kwa mfano Kiswahili kwenda lugha nyingine kama vile, Kijerumani “Kasri ya Mwinyi Fuad” (Dei Sklaverei der Gewiirze) iliyotafsiriwa na Manique Lutgens na Karin Boden (1997) miongoni mwa kazi nyingi zilizotajwa awali.

Historia ya jamii husika hueleweka kupitia kazi za tafsiri. Katika tamthilia ya Nitaolewa Nikipenda kwa mfano, tunaona historia ya taifa la Kenya tangu wakati wa ukoloni hadi wakati wa uhuru. Kwa hiyo hapa tunaelewa yale yote wananchi wa Kenya walipitia wakati wa ukoloni, kwa mfano katika uk. 32 mwandishi anaonesha adha walizopitia wananchi wa Kenya katika harakati za kupigania uhuru na baadaye wakafanikiwa.

Vilevile tafsiri husaidia kukuza fasihi ya lugha lengwa. Kupitia tafsiri fasihi ya lugha lengwa inanufaika na kuingizwa vipengele kadhaa vya lugha hususani misemo au methali ambazo hazikuwepo katika lugha lengwa. Kwa hivyo, kwa kutafsiri misemo hii lugha lengwa nayo pia itakuwa imenufaika na misemo hiyo, kwa mfano, katika “Nitaolewa Nikipenda”, msemo; “when axes are kept in a one basket they must necessarily knock agaist each other” umetafsiriwa kama;“vyuma vikiwa katika gunia moja havikosi kugongana” uk. 24. Kwa hiyo tunaweza kuwa tumeongeza msemo mwingine katika Kiswahili kupitia tafsiri hii.

Pia tafsiri hutusaidia kujua itikadi ya mwandishi na pengine itikadi ya jamii husika. Kwa muktadha wa tamthilia hii tunaona mwandishi, anapinga sana tamaduni na mtindo wa maisha ya kimagharibi ikiwa ni pamoja na dini za kigeni, lugha zao na mambo yote yaliyoletwa na wakoloni, uk. 5.

Ukitazama kwenye uga wa fasihi simulizi, utagundua kwamba tanzu zote za fasihi simulizi zimetafsiriwa katika lugha mbalimbali  ili kukidhi haja ya jamii lengwa. Tafsiri hizi sio tu kutoka aidha Kiingereza hadi Kiswahili la hasha! Zipo kazi chungu nzima ambazo zimetafsiriwa zikiwa ni pamoja na hadithi za aina mbalimbali ambazo zimetafsiriwa kutoka lugha ya Kiswahili hadi lugha za kiasili.

Mfano mwafaka ni hadithi ambazo  ni khurafa, hekaya, mighani, mazimwi, ambazo kwazo tunaweza kuzipata katika lugha tofauti tofauti kulingana na malengo ya mtafsiri na mtafsiriwa. Mfano tu mwafaka ni aina mbalimbali za kharafa ambazo zimetawala kwenye maandishi mengi sana ya fasihi simulizi ikiwa ni pamoja na Kichicheo cha Fasihi simulizi cha Wamitila , Fasihi simulizi kwa shule za sekondari pamoja na Msingi wa Fasihi simulizi cha Kitula Kinge’ei na Catherine N.M. Kisovi. Machapishi haya yamebeba kazi chungunzima ambayo baadhi imetafsiriwa kutoka lugha mbalimbali hadi Kiswahili au lugha za asili.

Changamoto katika kutafsiri matini za kifasihi ima andishi au simulizi

Tafsiri hizi hata hivyo zimeandamwa na changamoto si haba  katika kuhakikisha kuwa tunapata tafsiri faafu za kazi za lugha ya kigeni.

a.       Kwanza kabisa ni muhimu kufahamu kuwa, matini za kifasihi huwa tofauti kabisa na matini nyingine. Lugha ya kifasihi huwa tofauti kabisa na lugha ya kawaida na hii ndio haswa husababisha kuwapo na changamoto. Lugha ya kifasihi imetawaliwa na misemo, nahau, methali na tamathali za semi, vipengele hivi kimsingi ndio huunda lugha ya kifasihi. Na kwa hiyo mfasiri anapokuwa katika mchakato wa kufasiri matini za kifashi ni lazima akumbane na changamoto katika kufasiri vipengele hivi. Kwa mfano anaweza kukutana na methali au msemo ambao haupo katika lugha lengwa kwa hiyo katika mchakato wa kufasiri anaweza kukosa kisawe cha methali au msemo huo katika lugha lengwa na akaishia kufasiri kisisisi au kutumia kisawe ambacho hupotosha maana. Kwa mfano, methali “A rich man’s fart does not stink” imetafsriwa kama “Mashuzi ya tajiri hayachukizi”. Mfasiri alipata ugumu katika kufasiri methali hii ndio maana akaamua kufasiri kisisisi. Ikiwa mfasiri hatokuwa na taaluma ya kutosha juu ya fasihi, hataweza kufasiri kwa ufasaha misemo, mafumbo, nahau, tamathali za semi na hata miundo na mitindo inayotumika katika kazi husika, kwa hiyo kufasiri matini za kifasihi pia huhitaji utaalamu katika uwanja huo.

b.      Changamoto nyingine ni tofauti za kiutamaduni. Mambo kama dini, mavazi, mila na desturi. Kwa mfano, majina ya Kirusi huwa na maana yenye ujumbe mahususi, hivyo yanapofasiriwa katika Kiswahili hupoteza ile maana halisi na kupotosha ujumbe uliokusudiwa.

c.       Vilevile changamoto ya tofauti za kiisimu baina ya lugha mbili katika muundo wa sentensi na maumbo ya maneno. Kwa mfano muundo wa Kiingereza ni tofauti na muundo wa Kiswahili. Kuna maneno mengine ambayo sio rahisi kupata kisawe chake katika lugha nyingine, kwa hiyo mfasiri anapokutana na maneno kama hayo hupata changamoto kubwa.

d.      Pia changamoto nyingine ni kutoelewa mbinu mwafaka ya tafsiri husika, hivyo husababisha tafsiri kuwa tenge/mbovu. Hivyo basi, ni dhahiri kwamba si rahisi kupata tafsiri iliyosahihi kwa asilimia zote, isipokuwa tunaweza kupata tafsiri bora kama tu wafasiri wa kazi za kifasihi watakuwa na sifa stahiki. Kwa mfano, uwezo wa kumudu lugha, kujua utamaduni wa lugha husika pamoja na mazingira yake, kuwa na ujuzi wa taaluma husika kabla ya kufasiri nk.

e.       Kwa upande mwingine, ushairi ni utanzu unaokabiliwa na changamoto nyingi zaidi katika kufasiri kutokana na kwamba, kwa kiasi kikubwa ushairi hutumia lugha ya mkato na ya kisanaa zaidi yenye msamiati mgumu uliosheheni taswira, ishara, lahaja, tamathali za semi pamoja na misemo, mafumbo nk. Hivyo basi, kuna uwezekano mkubwa wa kupotosha maana ya kifasihi pamoja na sanaa iliyomo katika utanzu huu. Licha ya hayo, vilevile ugumu unasababishwa na kanuni za kiarudhi hasa katika mashairi ya kimapokeo kwani, ni vigumu sana kutafsiri ushairi huku ukizingatia urari wa vina na mizani bila kupotosha maana iliyokusudiwa.Upotoshaji wa kipengele cha mtindo ni tatizo lingine. Matini mengi ya kiingereza hasa hutumia neno “ACT” Neno hili hufasiriwa kama onyesho na vilevile kama tendo. Upotoshaji huu huleta mkanganyo hasa kwa msomaji wa matini pokezi. Huifanya hadhira ifikiri kwamba hivi ni vitabu viwili tofauti. Jalada ni sula jingine. Upotoshaji wa jalada la kitabu hufanyika kutokana na utamaduni wa lugha chanzi na lugha lengwa. Michoro hufanywa kwa kuzingatia kipengele cha utamaduni.

 

 

Suluhisho la changamoto hizi.

Changamoto hizi zote zinaweza kukabiliwa tu ikiwa;

·         Mtafsiri atakuwa na umahiri wa lugha zote.

·         Atazielewa tamaduni za jamii hizi.

·         Atafahamu mazingira ya tamaduni zote mbili.

·         Atajua lengo au dhamira ya mwandishi wa matini chanzi.

 

 

 

 

Hitimisho.

Kimuhtasari, makala hii imedadisi mchango wa kazi zilizotafsiriwa katika kuendeleza lugha na fasihi hasa simulizi  ya Kiswahili pamoja na kuchanganua changamoto zinazoambatana na tafsiri hizi. Imedhihirika wazi kuwa ipo haja ya kuzidhamini kazi hizi, kuzichunguza upya tena kwa nia ya kuzikosoa na zaidi ya yote kupendekeza njia mwafaka za kuibuka na tafsiri faafu katika karne hii ya teknolojia na utandawazi.

MAREJELEO

a.       Catford, J. (1965). Linguistic Theory of Translation. London: Oxford University Press.

b.      Crystal, D. (1987). Encyclopedia of Language. Cambridge: Cambridge University Press.

c.       Larson, M. (1994). “Translation and Linguistic Theory” An article in the Encyclopedia of Language and Linguistics. Vol.9 Pergamon Press Oxford.

d.      Mwansoko, H. (1996).  Kitangulizi cha Tafsiri: Nadharia na Mbinu. Dar-es- Salaam:  TUKI.

e.       Munday,  J.  (2001).  Introducing  Translation  Studies:  Theories  and     Application.  London: Routledge.

f.       Newmark, P. (1981): Aproaches to Translation. Oxford: London.

g.      Nida, E. (1964). Toward a Science of Translating. Leiden: E. J. Brill.

h.      Omboga, Z. (1986). Fasihi Tafsiri katika Ukuzaji wa Fasihi ya Kiswahili: Matatizo na Athari zake. Unpublished M.A Dissertation, Nairobi University.

i.        Teilanyo, D. (2007). `Culture in Translation: The Example of J.P. Clark`s The Ozidi Saga` in Babel, Vol:53, Issue:1. Pg. 79-82.

j.        TUKI, (2004).  Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Nairobi: Oxford University Press.

k.      TUKI, (2006). English-Swahili Dictionary. Dar-es-Salaam: TUKI

l.        Wanjala S. F (2011) Misingi ya ukalimani na tafsiri; Serengeti Education publisher (T) L.T.D. Mwanza Tanzania

m.    Method, S.(2015).Umahiri Katika Fasihi ya Kiswahi, Mwongozo Kwa Mwanafunzi na Mwalimu   wa Fasihi Simulizi na Andishi. Meveli Publishers (MVP).

n.      Ruhumbika, G. (1978). Tafsiri za kigeni katika ukuzaji wa fasihi ya Kiswahili. Makala.

o.      Wafula, R.M (1999).Uhakiki wa tamtiliya, Historian a maendleo yake . Nairobi Kenya: Jomo Kenyatta Foundation.


 

No comments:

Post a Comment