JADILI KAULI KUWA NENO NDICHO KIPASHIO CHA
KIMSINGI CHA SEMANTIKI
TUKI (2004) wanadai kuwa neno kama kipashio cha
usemaji ambacho hujengwa na mwanadamu au mkururo wa sauti zilizopangika
kisilabi na ambazo hutambuliwa na wasemaji wa lugha inahusika kuwa kitu kimoja
chenye maana mahususi.
Naye Mdee (2010:5) anafasili neno kwamba ni
mfululizo wa herufi ulioafungamana pamoja na kuzungukwa na nafasi tupu. Pia
Kihore na wenzake (2001) wanafasili neno kwa kutulia maanani maelezo ya Lyons
(1984:194-208) kuwa neno linaweza kufafanuliwa katika misingi ya kiumbo-sauti
(yaani, kwa kuchunguza sauti zinazounda umbo zima), kiotografia (yaani kwa
kuchunguza herufi zinazotumika katika kuliundika umbo lake) na kisarufi (yaani,
kwa kuchunguza kilekinachowakilishwa na umbo husika katika lugha).
Spencer(1991:41)
anafafanua kuwa dhana ya neno ni dhana tata sana
japokuwa ni dhana muhimu sana katika nadharia za
mofolojia.Wataalamu mbalimbali wamejaribu kufasili neno lakini
kila nadharia waliyoitumia kufasili neno haikukidhi
kueleza neno ni nini hasa ukitofautisha na dhana nyingine kama
leksikoni. Njia mojawapo ya kufasili neno ni kwa kuangalia sifa zake kiisimu
yaani kifonolojia, kimofolojia na kisemantiki. Ikiwa kigezo hiki
kitatumika kwa lugha moja moja huweza kuwa na mafanikio lakini
tatizo kubwa ni kupata vigezo majumui vitakavyokidhi lugha zote.
Katamba
(1993:17) anadai kuwa wazo kuwa lugha huundwa na maneno huchukuliwa kwa mazoea
ya watu wengi kwani hata mtu asiyejua kusoma na kuandika anatambua kuwa kuna
maneno katika lugha yake. Kumekuwa na mawazo tofautitofauti juu ya neno hasa ni
nini. Dhana ya neno hutumiwa katika fahiwa mbalimbali ambazo ni vigumu
kuzitofautisha.
Mdee
(2006:5) anadai kuwa umbo linalojulikana katika lugha ya kawaida kama neno lina
utata kwani ni umbo lenye sura nyingi. Utata huu unatokana na mitazamo tofauti
ya wanaisimu kuhusu kipashio hiki kitahajia, kimatamshi,na kimaana.
Kamusi ya Kiswahili Sanifu (toleo la tatu, 2013:420)
wametoa fasili tatu za neno. Fasili ya kwanza “neno” limefasiliwa kama
mkusanyiko wa sauti zinazotamkwa au kuandikwa pamoja na kuleta maana. Kisha
wakafasili neno kama jambo kubwa mfano nina “neno” nataka kukupa;
ameniletea neno, na katika fasili ya tatu wamefasili neno kama mahubiri, mfano
“neno” la Mungu.
Kwa mujibu wa Longman Dictionary (2008:1899)
wamefasili neno kama kipashio cha lugha ambacho mtu anaweza akaelewa
iwapo kitakuwa kimesemwa au kuandikwa kama kilivyo. (tafsiri yetu)
Habwe na Karanja (2004:71) wanasema neno ni kipashio
cha kiisimu kinachoundwa na mofimu moja au zaidi.
Katamba (1994:38) anasema neno ni kipashio kidogo cha
maana katika lugha ambacho kina dhima ya kisarufi. Anaendelea kusema, neno
linaweza kusimama peke na kuleta maana bila kupachikwa vipande vingine. Hivyo
katika neno “childish” (utoto) linaweza kutenganishwa na kubaki “child” (mtoto)
na neno hili likatumika kiupwekeupweke kwa sababu ni neno linalojitegemea.
Lakini hatuwezi kutenganisha kipande “ish” kikasimama pekeyake na kuleta maana.
Kutokana na maelezo haya basi neno ni kipashio cha lugha kinachoundwa na
mofu moja au zaidi ambayo inaweza kusimama peke yake na kuleta maana katika
lugha mahususi.
Ni kweli dhana ya neno ina utata. Utata huo
unasabishwa na vigezo tofautitofauti ambavyo hutumika katika kufasili dhana ya
neno na mipaka yake.
Mdee (2010:5) anafafanua njia tatu zinaweza kutumika
katika kufasili neno, njia hizo ni kama:- neno kama kipashio huru
kisichogawanyika; maana ya neno kiothografia, na neno kama kipashio cha maana.
Sisi tumeenda mbali kwa kuongeza fasili nyingine za neno kwa vigezo kama vile
kigezo cha kisarufi katika kufasili dhana ya neno na kigezo cha kifonolojia.
Neno kama kipashio
huru kisichogawanyika.
Fasili hii ya neno ni ya Leonard Bloomfield (1933)
inayosema “neno ni umbo dogo kabisa lililo huru”. Fasili hii ina mambo makuu
mawili, kwanza neno liwe umbo dogo, pili neno liwe umbo huru. Hapa umbo dogo
humaanisha umbo ambalo haliwezi kugawanyika bila kupoteza maana yake. Mfano
neno “pasi” huwezi kuligawanya katika “pa” na “si” bila
kupoteza maana yake. Hivyo umbo dogo ni lile ambalo linashikilia maana. Kwa
upande wa neno kuwa huru ina maanisha umbo hilo lazima liweze kutamkwa pekee
bila kutegemea au kuliambisha kwenye neno lingine, haya ni maneno kama
vile njoo, lete, jua, n.k.
Tatizo(utata) la kigezo hiki:
Ugumu wa kigezo hiki neno linalopewa uzito hapa ni
lile katika lugha za mazungumzo pekee. Katika lugha za maandishi tunaweza kuwa
na vipande vidogo vya maneno lakini ambavyo vikiwa huru hatuwezi kusema vina
maana kwa kuwa huwa havirejelei kitu au hali yoyote ile. Mfano katika lugha ya
Kiswahili vipande “na”, “kwa”, “tu”, n.k havina maana
vikiwa pekee pekee. Katika lugha ya Kiingeza vipande kama “a”, “the”,
“and”, “to”, n.k vivyo hivyo havina maana vikiwa pekee pekee.
Maana ya neno
kiothografia.
Kigezo hiki huchukulia neno kuwa ni maandishi
yanayoacha nafasi mwishoni. Rubanza(2010), anaeleza kwamba neno
kiothografia ni mfuatano wa maandishi ambao huacha nafasi tupu mwishoni bila
uwepo wa nafasi tupu katikati. Neno hudhiirika linapokuwa katika maandishi
tu na lisiwe na nafasi katikati. Mfano; ubao, chaki n.k.
Maneno kama Askari kanzu, Bata maji, n.k huchukuliwa
kama maneno mawili tofauti. Katika Kiingereza neno kama “cannot”, “blackboard”,
n.k huchukuliwa kama neno moja. Maneno kama “washing machine” (mashine
ya kufulia) na “White House” (ikilu ya marekani) huchukuliwa kama maneno
mawili tofauti.
Matatatizo ya kigezo hiki:
Hushidwa kuelezea maneno ambatani, kwao uandikaji wa
neno ambatani kwa kutenga au kuacha nafasi katikati huchukulia kuwa ni maneno
mawili. Hii sio sahihi kwani maneno ambatani huwa na dhana moja hivyo hutakiwa
kuchukuliwa kama neno moja. Pia kigezo hiki hushughuliki tu na lugha ya
maandishi na kuipuuza lugha ya mazungumzo ambayo ndiyo hutupatia lugha ya
maandishi. Pia zipo kugha nyingine ambazo hazitengi maneno yake katika
uandishi, pamoja ya kuwa ndani ya neno moja kunaweza kuwa na dhana nyingi
zinazorejelewa. Mfano lugha ya Kigreenland Eskimo neno “uluminippug” maana yake
ni “yumo mwanaume ndani ya nyumba yake”.
Dhana ya neno kifonolojia.
Kigezo hiki huchukulia neno kuwa ni kipande cha lugha
kinachotokana au kujengwa na kipashio kidogo cha kimatamshi. Kufuatana na
kigezo hiki kuna vigezo fulani vilivyo wekwa ambavyo hutofautiana kutoka lugha
moja na nyingine. Rubanza (ameshatajwa) hueleza kwamba zipo lugha ambazo upo
uwezekano wa kulitambua neno kwa kutumia sifa za kimatamshi. Lugha kama hizi ni
zile ambazo zina utaratibu wa kuweka mkazo mahali fulani maalumu katika maneno
wakati wote. Anaeleza zaidi kwamba sehemu hiyo inaweza kuwa mwanzoni mwa kila
silabi ya kwanza ya neno, au silabi ya pili toka mwisho kwa baadhi ya lugha.
Kwa mfano chunguza sentensi ifuatayo kutoka katika lugha ya Kingereza; “I
didn’t take the test yesterday”
Kufutana na utaratibu wa lugha hii sentesi hii ina maneno matatu tu
yaliyokolezwa, kwasababu mkazo huwekwa kwenye maneno yenye kubeba maana
(content words). Utaratibu huu una vighairi kwa sababu kuna wakati hata yale
maneno yasiyobeba maana (grammatical words) hubeba mkazo kwa sababu za
kimsisitizo wa neno au maneno husika katika sentensi (prosodic stress) Mfano
katika sentensi ilele “I didn’t take the test
yesterday” Ikiwa mzungumzaji ataweka mkazo kwenye “I” atakuwa akionyesha
msisitizo sio yeye aliyefanya jaribio jana. Ikiwa mzungumzaji
ataweka mkazo kwenye “didn’t”atakuwa anasisitiza kuwa yeye hakufanya jaribio
jana (labda kafanya jambo jingine). Na ikiwa mzungumzaji ataamua kuweka mkazo
kwenye “the” atakuwa akimaanisha kuwa hakufanya jaribio hilo(linalokusudiwa
na muulizaji) labda kafanya jaribio lingine tofauti.
Hivyo kwa kutumia kigezo cha mkazo katika maneno tunashindwa kufahamu neno hasa
ni lipi. Je vile vipande vya sauti ambayo havibebi maana katika lugha basi
navyo ni maneno? Na kama ndio, basi kwa nini lugha hii isivitambue kama ni
maneno kamili kiasi cha kubeba mkazo asilia?
Dhana ya neno kwa kigezo cha maana.
Kwa mujibu wa Mdee (ameshatajwa) hueleza kwamba neno
ni kipashio kidogo cha lugha chenye maana, hueleza zaidi kwamba neno ni lazima
liwe na maana. Mfano; baba – mzazi wa kiume, mama –
mzazi wa kike. Kwa hiyo kwa kutumia kigezo hiki neno hutambuliwa kuwa ni
kipashio cha kiisimu chenye maana.
Utata wa kigezo hiki: Je, maneno yote ya lugha yana
maana ya kisemantiki? Pia kuna maneno mawili au zaidi yenye maana moja, Kwa
mfano; mkono wa birika, maana yake mchoyo. Yapo maneno mengine
yenye maana zaidi ya moja, mfano; kaa, paa, na kata,
maneno haya yakisimama yenyewe huwezi kupata maana moja mpaka yawe katika
mahusiano na maneno mengine kwenye sentensi.
Dhana ya neno kisarufi.
Kwa mujibu wa Katamba (1993:19) ili neno litambulike
lazima liwe katika muktadha wa matumizi. Katamba, anasema neno moja linaweza
kuwa na dhima mbalimbali na dhima hiyo itagundulika tu litakapokuwa ndani ya
muktadha wa matumizi kwenye sentensi. Anatoa mtano wa neno la kiiingereza “cut”
kwamba likiwa kiupweke upweke mtu hawezi kutambua linarejelea nini, pamoja
kwamba neno hilo katika lugha ya Kiingereza ni kitenzi yaani “kata” lakini kuna
wakati linaweza kutumika kurejelea nomino. Chunguza mifano hii: “I need
my cut” na “I have cut my
finger”. Ukiichunguza vizuri mifano hii “cut” katika sentensi ya kwanza
hurejelea nomino yaani “nahitaji stahiki yangu”(tafsiri yetu) na “cut”
katika sentensi inayofuata hurejelea kitenzi yaani “nimekata kidole changu”.
Kigezo hiki pia
huenda mbali kwa kufafanua kuwa pia maneno kama; na, tu,si,
n.k katika Kiswahili na maneno; and, an, the,
on n.k katika Kiingereza nayo hayawezi kutambulika yanarejelea nini lazima
yawe katika muktadha wa matumizi ndio tunaweza kusema ni aina gani za maneno au
kutambua maana zake.
Udhaifu wa kigezo hiki ni kwamba kuna maneno mengi
sana ambayo maana zake hutambulika hata yasipokuwa katika muktadha wa matumizi
kwenye sentensi, aya au kifungu cha habari. Maneno haya ni kama vile nomino za
mahali kama vile Dar es Salaam, Ulaya, Bukoba n.k;
nomono za pekee zinazorejelea majina ya watu kama vileMutashobya, Mwendamseke, Rubanza,
n.k. Sasa tunajiuliza kuwa aina hizi za nomino na nyingine nyingi ambazo ni
kama hizi je si maneno? Hivyo na kigezo hiki hakijajitosheleza katika kutupatia
maana ya “neno” itakayokidhi mahitaji ya taaluma zote.
Kwa hivyo kutoka na makala haya ni kuwa kwa vile semantiki
ni tawi la isimu ambalo linashughulikia matumizi ya lugha katika awamu
mbalimbali na neno likiwa mojawapo wa viambajengo hivi, neno linakuwa nguzo na
msingi katika tawi hili. Neno linakuwa na nafasi ya kimsingi ni wazi kwamba
suala hili zima linajengeka kwenye misingi ya neno.
Kimsingi neno linaweza kujitokeza kama mofu,
au mofimu linapotekezea majukumu yake.
Neno kama mofu.
TUKI(1990),
katika Dafina ya Lugha wanasema kuwa, “Mofu ni kipashio cha isimu maumbo
kiwakilishacho mofimu”. Massamba (2004), katika Dafina ya Lugha anasema , Mofu
ni kipashio cha kimaumbo ambacho huwakilisha mofimu. Kwa mujibu wa Nida (1949),
wanasema, Mofu ni umbo la neno ambalo huwakilisha mofimu na ambalo huthihirika
kifonolojia na kiothografia. Mofu ni kipashio kidogo kabisa chenye maana katika
lugha.Mofu hawezi kugawanywa katika sehemu ndogo zaidi bila kuharibu maana
yake. Mofu huwakilisha maana za kileksika na zile za kisarufi. (Platt,1985).
Kwa ujumla, Mofu ni kipashio cha kimofolojia ambacho husitiri maana za mofimu
katika lugha na huweza kudhihilika kifonolojia zinapotamkwa na kiothografia
zinapoandikwa katika lugha. Mofu huainishwa kwa kuzingatia vigezo viwili;
Kigezo cha maana zinazowakilishwa na mofu na Kigezo cha mofolojia ya mofu.
Mofu huainishwa kwa
kuzingatia vigezo viwili:
(i) Kigezo
cha maana zinazowakilishwa na mofu;
(ii) Kigezo
cha mofolojia ya mofu.
Tunapotumia kigezo cha
maana zinazowakilishwa na mofu, tunapata aina tatu za mofu, yaani:
(i) Mofu
huru
(ii) Mofu
funge
(iii) Mofu
tata
Kwa upande mwingine
tunapotumia kigezo cha mofolojia au maumbo ya mofu zenyewe tunapata aina mbili
za mofu, yaani:
(i) Mofu
changamano
(ii) Mofu
kapa
Kwa mantiki hii tunazo
aina tano za mofu ambazo ni:
(i) Mofu
huru
(ii) Mofu
funge
(iii) Mofu
tata
(iv) Mofu-changamano
(i) Mofu
Huru
Mofu huru ni zile mofu
ambazo zinaweza kukaa peke yake kama maneno kamili yenye maana inayoweza
kueleweka bila kusaidiwa na mofu nyingine. Aghalabu, mifano mingi ya mofu huru
hupatikana kutoka kwenye vipashio vya lugha, kama ifuatavyo:
(a) Nomino: {baba},
{kuku}, {sungura}, {ndege}, {dada}, {paka}, nk.
(b) Vivumishi:
{safi}, {baya}, {dhaifu}, {zuri}, {imara}, {hodari}, nk.
(c) Viwakilishi:{mimi},
{sisi}, {wewe}, {ninyi}, {yeye), {wao}, nk.
(d) Vielezi: {upesi},
{haraka}, {sana},
{leo}, {jana},
{juzi}, nk.
(e) Vitenzi:
{tafiti}, {samehe}, {arifu},
{sali}, {jibu}, {badili},
nk.
(f) Vihusishi:
{ya}, {juu}, {mbele}, {kwa}, nk.
(g) Viunganishi:{na},{halafu},
{bado}, {ila}, {aidha},{pia}, nk.
Kwa mujibu wa mifano hii
inadhihirika kwamba Kiswahili kinazo mofu huru nyingi ambazo zimo katika aina
zote za vipashio vya lugha. Hivyo, mofu huru ni mofu ambazo zinaweza kukaa peke
yake kama maneno kamili yanayoeleweka bila kusaidiwa na viambishi.
(ii) Mofu
funge au Mofu tegemezi
Mofu funge au Mofu
tegemezi ni mofu ambayo haiwezi kutumiwa peke yake kama neno lililo na
maana yake kamili; aghalabu mofu funge hutumiwa kama kiambishi tu
kinachoambatanishwa na mzizi au viambishi vingine ili kulikamilisha neno
husika. Mofu funge ina sifa zake ambazo ni pamoja na:
(a) Mofu
funge haiwezi kukaa peke yake ikawa neno kamili.
(b) Mofu
funge ni lazima iambatanishwe na angalau mafu nyingine moja ndipo tupate neno
kamili.
Kutokana
na sifa hii ndiyo mdiyo maana wanaisimu wengine huziita mofu hizi kuwa ni mofu
tegemezi ambayo ina maana sawa na mofu funge
Neno kama mofimu
Mofimu ni vipashio vinavyoonyesha uhusiano uliopo kati ya
sauti-msingi za lugha (yaani fonimu) na maana maalumu katika sarufi ya lugha.
Hivyo tunaweza kusema kuwa mofimu ya umoja katika neno {mtu} imeundwa
na fonimu /m/ ambayo ni king’ong’o cha mdomo; na mofimu ya wingi imeundwa na
fonimu mbili /w,a/ ambazo ni kiyeyusho na irabu chini. Sasa bila shaka unaweza
kuona uhusiano uliopo kati ya vipashio vya kifonolojia tulivyojadili katika
sura ilyotangulia, na uundaji wa mofimu za lugha.
Kila neno katika lugha limejengwa na
mofimu moja au zaidi. Neno linalojengwa na mofimu moja tu linaitwa neno
sahili, na lile linalojengwa na mofimu zaidi ya moja linaitwa neno
changamano. Hivyo, katika Kiswahili, tunaweza kusema kuwa {chungwa} ni
neno sahili kwa vile haliwezi kukatwakatwa katika vipashio vidogo zaidi, kama
tukilinganisha {chungwa: machungwa}.
Maneno yaliyo mengi katika lugha kama ya Kiswahili ni
changamano kama itakavyodhihirika katika mifano. Hata maneno mafupi kama {wa,
ya, vya} ya sentensi za (4) hapo juu, ni changamano. Kila moja lina
mofimu mbili, moja ambayo inasimamia upatanisho na nomino, na /-a/ ambayo
haibadiliki, na katika sarufi ya Kiswahili tunaiita {-a} mofimu ya ‘uhusiano’.
Lugha nyingine zinayo maneno sahili mengi zaidi ya Kiswahili. Katika lugha ya
Kiingereza, kwa mfano, nomino nyingi katika umoja ni manerio sahili: {boy,
girl, book} etc. Lakini, katika wingi, nomino nyingi za Kiingereza ni
maneno changamano {boy-s, girl-s, book-s} etc. Hata vitenzi
vya Kiswahili si maneno sahili hata kama hayajaambikwa vipashio vingine. Kwa
mfano neno {sema}:
8 a)
Juma amesema wageni wamekuja
b) Juma hasemi uwongo.
Kipashio /sem-/ katika sentensi hizo ni mzizi wa
kitenzi {sema}, kwa sababu ndiyo sehemu ambayo haibadiliki, na
hivyo tunaona kuwa fonimu /a/ ya {sema} si sebemu ya mzizi wa
kitenzi hicho kwa sababu inaweza kudondoshwa na nafasi yake ikacbukuliwa na
kinashio kingine kama hapo juu. Hata hivyo tunaweza kupata maneno zaidi ya
Kiswahili ambayo ni sahili, kama vile maneno ya sifa: {safi, kubwa,
dogo, fupi; zuri} n.k. (mfamo:{chungwa safi, kubwa, zuri} n.k.
Neno changamano linaundwa na aina mbili za mofimu:
mzizi na kiambishi (au viambishi);
ambapo neno sahili linaundwa na mzizi peke yake. Viambishi viko vya aina
tatu: viambishi-tangulizi, vinavyoambikwa kabla ya mzizi wa
neno; viambishi-fuatishi, vinavyoambikwa baada ya mzizi;
na viambishi-kati, ambavyo vinaingizwa katika mzizi, na hivyo
kuukata katika sehemu. /m/ na /wa/ katika maneno {m-tu} na {wa-tu} ni
viambishi-tangulizi, ambapo /-i-/ na /-ish-/ katika maneno {kat-i-a} na {kat-ish-a) ni
viambishi-fuatishi. Viambishi kati havitokei katika Kiswahili, lakini vipo
katika lugha nyingine.
MAREJELEO.
Bloomfield,
L. (1933). Language. Henry Holt: New York.
Habwe, J. na Karanja, P. (2004). Misingi ya
Sarufi ya Kiswahili. Phonex Publisgers: Nairobi
Katamba, F. (1993). Morphology. Mac Millan
Press Ltd: London
Katamba, F. (1994). English Words.
Routledge: London
Mdee, S. (2010). Nadharia na Historia ya
Leksikografia. TUKI: Dar es Salaam
Quirk, L. (2005). Longman Dictionary of
Contemporary English. Pearson Longman: New York
Rubanza. (2010). basic Reading.
Yaliyoandailwa na Rubanza.
TUKI (2013). Kamusi ya Kiswahili Sanifu.
(Toleo la tatu). Oxford: Dar es Salaam
Besha,
R.M. (2007). Utangulizi wa Lugha na Isimu. Dar es Salaam: Macmillan
Aidan Ltd.
Habwe,
J. & Karanja, P. (2007). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili.
Nairobi: Phoenix Publishers.
Katamba,
F. (1993). Morphology. London: Macmillan Press Ltd.
Massamba,
D.P.B na Wenzake. (2013). Fonolojia ya Kiswahili Sanifu.
Dar es Salaam: TUKI.
Matinde,
R.S. (2012). Dafina ya Lugha Isimu na Nadharia: Kwa Sekondari, Vyuo vya Kati
na Vyuo Vikuu. Mwanza: Serengeti Educational
Publishers (T) Ltd.
Mdee,
D. (2007). Nadharia za Leksikografia. Dar es Salaam: TUKI.
TUKI.
(1990). Kamusi ya Isimu na Lugha. Dar es Salaam: TUKI