Monday

uhakiki watamthiliya ya mashetani nadharia ya kibrechrian pdf

0 comments

 

UHAKIKI WA TAMTHILIA YA MASHETANI KWA KUTUMIA NADHARIA YA KIBRECHTIAN

Nadharia hii ya Kibrechtian iliasisiwa na Bertolt Brecht ambaye alikuwa sogora wa michezo ya kuigiza.Mwandishi wa michezo ya kuigiza Bertolt Brecht alizaliwa mwaka 1898 Ujerumani  katika mji wa  Augsburg. Baada ya kutumikia kama utaratibu wa matibabu katika Vita vya Kwanza vya Dunia na kushangazwa na madhara ya vita, alikwenda kwanza Munich na kisha Berlin akitafuta kazi katika kumbi za  michezo ya kuigiza. Kipindi hicho cha maisha yake kilimalizika mwaka wa 1933 wakati Nazi walipoanza kutawala Ujerumani. Brecht alihama na kukosauraia mwafaka.

Katika kazi yake ya jukwaani, Brecht aliivumbua nadharia ya Bretch/Alienation. Hii ni nadharia ambayo inajaribu kumtenga mtaamaji wa mchezo wa kuigiza na hali halisi ya mambo namna yalivyo. Kwa hakika utagungua kuwa, watazamaji wa mchezo wa kuigiza huwa  wanakosa kutofautisha mhusika na uhusika wake au kazi yake katika mchezo wa kuigiza.
Kwa wakati mwingine utagundua kuwa wale watazamaji mara nyingi huwahusisha wahusika na nafasi wanazozishughulikia katika kazi yoyote ya fasihi. Kwa mfano wakati mhusika anapocheza nafasi ya kuwa mchawi, hadhira au watazamaji hustahili kumtenga mhusika huyu na uchawi. Ingawa pia wapo wale wahusika ambao nafasi zao katika mchezo wa kuigiza huathiri hali zao za maisha. Huenda utakumbana na mhusika aliyekuwa mchawi katika kazi ya sanaa, akiwa mchawi halisi wa maishani mwake.
 
Ili kutafiti hili,Brecht alitumiambinu mbalimbali za kutimiza hili. Mbinu zizihizi zinajitikeza mojakwamoja katika tamthiliaya Mashetan .Wanasarakasi wengi hupenda wanawatenganisha watazamaji wa mchezo jukwaani na wahusika. Kwa upande wake Brecht alikuwa na lengo la kuwateka nyara wataamaji wa mchezo wa kuigiza kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Kwa kutekeleza hili, Brecht alitumia mbinu mbalimbali za kihisia.
 
Mbinu hizi ni pamoja na ni ile hali ya kuwakumbusha watazamaji kuwa wanautazama mchezo wa kuigiza.Ukirejelea tamthilia ya Mashetani utagundua kwamba ukitazama katikautangulizi wa kila onyesho, vipovitangulizi ambavyo humwelekeza msomaji na kumfanya afahamu mahali aliko na kule anakotarajiwa kusafirishwa na kazi ya fasihi husika.Hii inadhihirika wazi tunapotazama vitangulizi hivi:-Sehemu ya kwanza:-Mbuyu wenye pango.Vijana wawili katika matembezi yao wanafika mbele ya mbuyu huo- Hapo moja kwa moja mtazamaji au msomaji wa kazi hii huelewa fika kinachostahili kuangaziwa na humpawakati mwafaka wa kuweza kung’amua na kujiweka katika hali ya ange kwa kuwa na taharuki kuhusiana na vitangulizi kama hivyo.
  
Mbinu ya pili ni usimulizi/naratolojia. Nadharia hii inahusiana na usimulizi wa hadithi. Hadidhi ni fabula inayoelezewa kwa mtiririko wa kimantiki unaosimulia kuhusu tukio fulani. Prince anafafanua dhana ya simulizi kama uelezaji wa tukio moja au mengi ya kihalisia au kibunilizi.Kulingana na maelezo ya Gérard Genette, simulizi ni mfuatano halisi au ya kibunulizi ambayo ni kiini au yanayolengwa na usemi fualni. kulingana naye, simulizi huhusisha utambwaji wa matukio. 
 
Nadharia hii huchunguza sifa zinazohusisha simulizi na kuzitenganisha nyingine. Msingi wake umewekwa na Mwanafalsafa Plato ambaye anadai kuwa usimuliaji hulingana na udhihirishaji. Plato anazua vipengele viwili ambavyo ni mimesia na digesia. Katika mimesia mtunzi hajitokeza waziwazi kama msemaji ilhali katika digesia msemaji anaweza kutambulika na hadhira yake. pia Mtaalamu Lord Raglan katika kazi yake ya The Hero iliyosheheni maiasha ya mashujaa wa kitamaaduni kama vile Oedipus, Robi Hood amechangia sana katika kukua kwa nadharia hii. Anaeleza kuwa lazima kuwe na mfuatano maalum wa matukio katika uandishi kama vile kutabiriwa kwa kuzaliwa kwa shujaa, kuzaliwa kwake, maajabu yake, ukombozi wake na hatimaye kifo chake kutokana na usaliti.
Wahakiki wa kinaratolojia wamebainisha dhana mbili katika usimulizi; wakati hadithi na wakati matini. wakati hadithi ni wakati inaochukua hadithi husika kuanzia mwazo hadi mwisho. Wakati unaweza kueleweka kwa urahisi kwa kuwa unaweza kuwa baina ya siku moja, miezi mitatu au miaka mingi inayohusisha vizazi. Dhana ya wakati matini ni wakati inayochukua wakati fulani kusomwa. Wakati huu ni vigumu kutathminiwa ila itategemea muda atakaouchukua msomaji na kasi yake. Hali kadhalika, kuna wakati ambapo wakati matiniunakuwa mrefu ukilinganishwa na wakati hadithi. Hili limejitokeza katika hadithi ya S. A Mohammed ya Kiza katika Nuru, ambapo Mvita amefika ofisini na hajatenda lolote bado kwa muda mrefu ilhali msomaji anaendelea kusoma.
Nadharia ya naratolojia hujikita katika kipengele cha wakati ambacho huangaliwa kwa kuvichunguza vigezo kama vile mpangilio, muda na idadimarudio. Katika kigezo cha mpangilio, matukio huweza kusimuliwa katika mfuatano wa kiwakati ama kwa kutofungamana. yasimuliwapo kiwakati, msuko na hadithi huwa huwa na mapangilio sawa. Kwa upande wa muda, hujiita katika uhusiano katika hadithi na kipindi ambacho kimechukuliwa, kipindi kirefu au kifupi? Muda katika nadharia ya naratolojia hujitokeza katika jinsi tano;-
 
Kwanza, muhtasari ambapo muda wa usemi/matini(usomaji) unachukuliwa kuwa mfupi kuliko ule wa hadithi. Kulingana na Rimmon-Kenan kasi ya hadithi huharakishwa katika muhstasari itokanayo na ufupishwaji wa muda fulani kwa kauli chache. udondoshaji ni dhana nyingine ambayo hurejelea pale ambapo maelezo fulani yameachwa katika matini fulani, (mwanda nunge wa kimatini) ilhali hadithi yenyewe ina wakati fulani. Katika hali hii wakati hadithi na wakati matini huwa tofauti. 
 
Vilevile onyesho ni dhana nyingine ambayo huleta sifa ya uigizaji katika matini yoyoyte ile. Katika dhana ya idadimarudio au umara wahakiki wa naratolojia hurejelea mara ambazo matukio hutokea katika hadithi au mara ngapi matukio hayo yanasimuliwa. Wananaratolojia wamebainisha aina tatu za urudiaji kama vile, tukio lililotokea mara moja linaweza kusimuliwa mara moja, pia tukio lenyewe laweza kusimuliwa mara kadhaa na panakuwa na urudiaji wa kisimulizi na hatimaye tukio likitokea mara kadhaa linasimuliwa mara moja. Uhakiki wa kinaratolojia huwaangalia wahusika kama kipengele muhimu cha matini ya kifasihi. Katika kuwabainisha wahusika, kuna uelezaji wa moja kwa moja ambapo maelezo ya wazi wazi kumhusu mhusika yanatolewa na mwandishi. Kwa mfano katika Rosa Mistika maelezo kuhusu yanatolewa waziwazi na mwandishi.
 
 Katika uwasilishaji usio wa moja kwa moja unahusisha matendo ya wahusika, maneno yao, sue zao, mandhari au hali zao. Msomaji huangalia jinsi wahusika wamewasilishwa na mandishi na kuwatambua. Kipengele kingine cha uhakiki huu ni mtazamo wa mhakiki/mtambaji. Mwandishi huwa na mtazamo fulani kuhusu maswala kadhaa na ambao labda angetaka amshirikishe msomaji. Nadaria ya naratolojia inahusiana na mwelemeo wake mkuu kwenye muundo wa kazi bila kuhusisha na muktadha wa kihistoria, kijamii, kisiasa au kitamaduni wa kazi zenyewe.
 
Kulingana na Brecht naratolojia  hutumiwa kuwakumbusha wasikilizaji kuwa wanautazama mchezo wa kuigiza. Mwelekezi huenda akawakumbusha kilichotokea au kitakachotokea mbeleni.Kwa hivyo natarolojia hapa huwe kielekezo kwa watazamaji iliwazidi kuwa na hamu ya kutazama au kuchora picha ya matarajio yao wakatiwa kuutazama mchezo wa kuigiza.
 
Mbinu hii  vile vile imetumika pakubwa katika tamthilia ya Mashetani. Tunathibitisha kuwa katika tamthilia hii, mwandishi huyu ameitumia kwa ukamilifu sana. Hii inathihirikakatika namna---
 
 
 
Njia nyingine ni kuzungumza moja kwa moja na hadhira.Hali kama hii vilevile huishirikisha hadhira mojakwa moja kwenye ujenzi wa kazi husika ya kifasihi hasa tamthilia. Kwenye Tamthilia ya Mashetani, Katika utangulizi sehemu ya kwanza, sura ya kwanza, mhusika Juma anakuwa na haya ya kusema kwa hadhira:-
 
Juma:-Wananchi; kwa mara nyingine chini ya mbuyu huu mimi Juma na rafiki yangu Kitaru, tunakuonesheni mchezo wa Shetani na Binadamu. Mimi nitakuwa Shetani na Kitaru atakuwa Binadamu.
 
Usimulizi huu mojakwamoja unaiweka hadhira au msomaji katika hali ya taharuki kwa kutaka kufahamu lengo mahususi la kutumia Shetani na Binadamu kama wahusika katika kazi hii. Watazamaji au wasomi wa kazi hii huwa na mshawasha wa kutaka kufahamu iwapo upo usabihiano wa kitabia kati ya uhalisia wa wahusika hawa na majina ya uigizaji(Shetani na Binadamu) 
 
Katika tamthilia neno hili Shetani limejitokeza katika hali mbalimbali. Shetani linatumiwa kuonyesha kiumbe aliyejawa na kiburi, uchoyo na ukatili.Anamwambia Binadamu kuwa:-
Mimi Shetani,
Siyo jini wala kuhani
Mimi shetani.
Uwezo wangu hauhifadhiki.
Wema wangu hauhisabiki
Ubaya wangu hausemeki
Ninajenga.
Ninabomoa.
Ninadhalilisha nitakavyo
Kwa kupitia haya ni dhihirisho kuwa usimuliziuliojitokeza hapo mwanzoni ni ishara tosha kuwa taharuki ambayo mtazamaji anakumbana nayo inajibiwa na matendo mbalimbali yanayojitokeza kadri mchezo unavyoendelea kuhusu tabia za shetani.
 
Njia ntingine huwa ni matumizi ya nyenzo mbalimbali katika mchezo wa kuigiza. Hizi huenda zikawa kadi teule.Nyenzo hizi sio tu hutewezesha kujua au kuifahamu tu kazi ya fasihi bali hutupa uelewa wa ndani kabisa . Kwa mfano ikiwa unatazama majibishano na mabishano  kati ya mume na mke na mhusika wa kike ainue bango au kadi isemayo “nimekorogeka” ile haiwezi kutuelewesha vilivyo kuhusu hali halisi ya familia kulingana na tabia za mhusika teule.Hata hivyo, ikiwa kadi itaandikwa “ nina mpango mbadala au sijawahi kumpenda” hali kama hii itawawezesha watazamaji kuelewa kwa undani asili na upeo wa misukosuko katika ndoa husika.
 
Katika kazi hii mtunzi ametumia vitu mbalimbali kijazanda ili kukamilisha kazi yake ifaavyo. Jazanda ni mbinu inayoelezea jambo fulani kwa kutumia lugha ya kimafumbo au lugha fiche. Inapotumiwa, kile kinachorejelewa huwasilishwa kwa lugha isiyokuwa ya uwazi (King’ei 1987, Njogu & Chimerah 1999, Wamitila 2008). Kwa hivyo ujumbe unaowasilishwa huwa katika maneno yaliyotumiwa kuashiria jambo jingine.
Jazanda ya abiria ni taashira ya raia wa mataifa machanga ya Kiafrika. Raia hawa hushurutishwa kwenda kule wanakoelekezwa na nguvu za kibepari (mkondo). Kwa hivyo hawana uhuru wa kujiamulia ni upande upi wauelekee. Kadhalika ingawa kila taifa lina kiongozi wake, viongozi hao hawana uhuru wa kuendesha mataifa yao jinsi wanavyotaka. Badala yake wanaagizwa lipi wafanye. Hivi ndivyo Kitaru anavyomaanisha akisema:
KITARU: […] toka tumepata uhuru, sisi Waafrika hapa imekuwa tumeingia … ehe, mfano mzuri … imekuwa kama tumeingia … katika jahazi moja zuri na jina letu limeandikwa. Lakini … nahodha … nahodha nani? […] je mkondo ukiwa unavutia upande mwingine, na nahodha anataka kupeleka jahazi upande mwingine? (Mashetani: 21)
Jazanda ya Bahari Kuu na Mkondo imetumiwa dhana ya bahari kuashiria ulimwengu unaomilikiwa na nguvu za kibepari. Kwa mfano, Kitaru anaeleza kuwa:
 
“Hadithi ya chewa. Mbali sana, ukivuka bahari saba, kuna chewa mkubwa. Chewa huyu akivuta pumzi maji yote yanakupwa, maji yote yanaingia kinywani mwake. Anaweza kutoka huko aliko, kuivuta na kuimeza mashua yoyote anayoitaka. Mashua inavutwa tu na mkondo wa maji, ikitaka isitake. Na huyu chewa siyo chewa bali ni shetani.” (Mashetani: 28) 
 
Eneo hili kubwa la maji hukusanya pamoja samaki wa aina nyingi kama vile chewa, papa, vidagaa, mkizi, nyangumi na wengineo. Watunzi wa tamthilia hizi mbili wametumia maisha ya baharini kumulika maisha halisi katika ulimwengu wa kiuchumi unaomilikiwa na mabepari. Viumbe wakubwa wanaoishi baharini kama vile chewa na papa ni viashiria vya madola makuu ulimwenguni. Jinsi samaki hao wanavyodhihirisha nguvu na uwezo wao mle baharini, ndivyo madola makuu ulimwenguni huwafanyia mataifa machanga katika maisha ya kiuchumi na kisiasa katika ulimwengu halisi wa binadamu. Jinsi samaki hao wanavyowahangaisha vidagaa mle baharini ndivyo mataifa makuu huyahangaisha mataifa machanga.
 
Mkondo ni njia ya maji katika bahari inayopitisha maji kwa kasi na kwa nguvu. Katika tamthilia hii, mkondo ni taashira ya nguvu za kibepari zinazomiliki uchumi na siasa za ulimwengu mzima. Kwa mfano, katika tamthilia ya Mashetani, jahazi hudhibitiwa na nguvu za mkondo ambazo huamua ni upande upi jahazi lile lipelekwe. Nguvu za mkondo huu hutatiza lengo la nahodha ambaye mwishowe huishia kulipeleka jahazi lile upande asiotaka ambapo yeye wala abiria 
 
 KITARU: […] toka tumepata uhuru, sisi Waafrika hapa imekuwa tumeingia … ehe, mfano mzuri … imekuwakama tumeingia … katika jahazi moja zuri na jina letu limeandikwa. Lakini … nahodha … nahodha nani? […] je mkondo ukiwa unavutia upande mwingine, na nahodha anataka kupeleka jahazi upande mwingine? (Mashetani: 21)
 
Ugonjwa wa Kitaru pia una dhamira fulani fiche. Ugonjwa wa Kitaru unaelezwa na wale anaoingiliana nao kuwa ni ugonjwa wa mashetani, mizuka, wasiwasi, machofu ya akili au kuendekeza akili. Ugonjwa huu ni jazanda inayoashiria mgongano wa nafsi zake mbili zinazokinzana. Hali hii inamwingiza kwenye mtafaruku mkubwa wa kiakili na kumfanya awe na fikira zinazogongana na kuzozana. Kwa hivyo ugonjwa wa Kitaru ni fikira alizonazo kuhusu vile anavyoweza kutoka katika hali hii ya ukabaila na kisha aweze kujenga uhusiano ulio na maana.        
 
Mbinu nyingine huwa ile ya mhusika mmoja kucheza sehemu zaidi ya moja katika mchezo wa kuigiza. Mabadiliko katika mhusika kama huyu hujitokeza kupitia mabadiliko katika sauti, matembezi ya mhusika, lugha ya ishara-mwili ambapo hadhira hugundua kuwa mhusika yule awasilisha sehemu mbili tofauti. Hii ina maana kuwa hadhira huandamana sako kwa bako na mhusika hivyo basi kugundua mabadiliko yoyote  katika mhusika yeyote yule. Katika tamthilia ya Mashetani tunwaona wahusika wakuu, Juma na Kitaru wakibadili uhusika kama Binadamu na Shetani. 
 
Katika hali hii ni mtazamaji au msomaji wa usanii huu ambaye anaweza. Tamthilia ya Mashetani imeonyesha wazi hali kama hii. Tunaona kupitia kwa wahusika wakuu ambao ni Juma na Kitaru kwamba wawili hawa wanacheza kuwa wahusika wawili tofauti.Juma anacheza kama Shetani naye Kitaru kuwa Binadamu huku wote wakiwa wanafunzi katika chuo kikuu ingawa wenye misimamo tofauti kuhusu maisha.
                                                                           

Pia kuna matumizi ya nyezo moja katika. Katika hali kama hii nyenzo moja inaweza kutumika katika miktadha mbalimbali. Kwa mfano kibeta kinaweza kutumika kama dawati, mlango wa gari au hata bomu. Katika tamthilia vifaa mbalimbali vimetumika kudhihirisha vitu mbalimbali.  Kwa mfano pango limetumiwa kama mafichoni na pia mahali pa kujiliwazia katika kucheza mchezo huo.

 Brecht vilevile aliamini sana katika matumizi ya taa ua mwangaza.Aliamini kuwa taa zikitumika kwenye jukwa, huwafanya wataamaji kuelewa barabara na kufahamu fika swala linaloangaziwa. Hata hivyo sanaa hii katika nyakati hizi wasanii wengi hutumia taa mbadala ambazo humwekamweka tu kila pande ya jukwaa.

 

Hitimisho

Kutokana na uchambuzi ulioko hapa ni dhahiri shahiri kuwa nadharia hii ni faafu mno katika uhakiki wa tanthilia ya Mashetani. Kulingana na mwasisi wake ambaye ni Brecht kama alivyoyaweka mawazo yake pamoja ni kuwa vipengee alivyoviangazia katika utafiti wake kwenye ukumbi wa michezo ya kuigiza vinajitokeza wazi katika tamthilia hii ya mashetani.

 

 

 
Michezo ya a Brecht bado imenoga sana katika nyakati hizi. Ikiwa unahitaji kuchunguza utendaji wa Brechtian, haitakuwa tofauti sana na mapitio mengine yoyote, isipokuwa kuwa utakuwa na nia ya kufahamu  jinsi wahusika wanavyoucheza mchezo husika kutokana ma maelekezi maalum. Kama mwandishi wa kisiasa, Brecht kwa hakika angetarajia uchezaji wa michezo hii wa kisasa  kushughulikia masuala  ibuka katika jamii huku mchezo ukibaki katika hali yake ya uhasalia.

 

Marejeleo.

a.     Bekson, Karl and Ganz, Arthur: Literacy Terms: A Dictionary (Calcutta: Rupa and Company, 1991).

b.     Brecht Bertolt: Shriften Zum Theatre (Frankfurt: 1959).

c.       Brecht Bertolt: Uber gegenstandslose Malerel, Uber Politik and Kunsl ed. Werner Hecht,( Frankfurt: Suhrkamp, 1997).

d.     Elsom John: Post War British Theatre (London: Routeledge and Kegan Paul, 1979).

e.       Eysteinssor Astoadur: The Concept of Modernism (London: Cornell Uni. Press, 1990).

f.        Karnad Girish: Author’s introduction, Three Plays (Delhi: Oxford University Press. 1994),

g.      Kulkarni V. L. , Dnyaneshwar, Kale K.N: Samiksha: Marathi Natak and Marathi
Rangabhumi ( Mumbai:Popular prakashan, 1963).

h.      Politzer Heinz: How epic is ‘Bertolt Brecht’s Epic Theatre’
Modern Drama” ed. Travis Bogard and William Oliver,( New York: Oxford University Press,

i.       1965).

j.       Willet John: The Theatre of Bertolt Brecht (London: Methuen & Co. Ltd., 1996).

k.     Williams Reymond: Drama from Ibsen to Brecht (London: Chtto and Windus, 1971).

l.       Kimani N. Na Chimera, R. (1999).Ufundishaji wa fasihi, nadharia na mbinu.Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.

m.  Rajmund Ohly, (2005). Historical Approach to Swahili Literature.An Open Question. Kiswahili Juzuu la 68. Dar es Salaam:TUKI

n.     Wafula R. M. na Kimani, M (2007). Nadharia za uhakiki wa Fasihi.Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.

o.     Hussein Ebrahim, (1971). Mashetani. Nairobi: O.U.P.

No comments:

Post a Comment