MWANDISHI WETU BAGAMOYO


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Ummy Mwalimu amewaagiza wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wote nchini kuhakikisha wanasimamia suala la wanafunzi kupumzika  wakati wa likizo  ili  kuwapatia watoto muda wa kujifunza masuala mengine ya Kijamii.


Waziri Ummy ameyasema hayo leo baada ya kupata maelekezo ya kisera kutoka kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknojia Profesa Joyce Ndalichako ambaye amemtaka kulisisitiza suala hilo  ili wanafunzi hao waweze kupata muda  wa kupumzika kipindi cha likIzo


Akihutubia kwenye Mahafali ya 29 ya  Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) Bagamoyo Waziri Ummy amesema watoto wanatakiwa kupumzika majumbani kipindi cha likizo ili waweze kusaidia kufanya kazi ndogondogo nyumbani, kusoma dini na kusaidia kufanya biashara ndogo za kuwasaidia wazazi pale wanapokuwa likizo.


“Sasa hivi elimu imegeuzwa kama biashara, watoto wamekuwa wakisoma masomo ya ziada  mpaka  kipindi cha likizo, hawapumziki, pia wazazi  huchangia fedha fedha kwa ajili ya masomo hayo, ya ziada, watoto hawafaulu kwa kusoma muda mrefu,  hivyo nawaagiza wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wanalisimamia hili” amesisitiza  Waziri Ummy


Amesema Serikali imepanga muda wa vipindi  wa masaa nane, ikiamini  muda huo wanafunzi wataweza kujifunza kwa kina masomo yote yaliyopangwa kwa siku, hivyo amewataka Wakurugenzi kuwaelekeza wakuu wa shule  kusitisha masomo ya ziada mpaka saa mbili  usiku, jumatatu hadi jumapili naagiza kusitishwa  mara moja kwa kuwa hatuwajengi watoto,tunawaharibu kwa kuwachosha kusoma muda wote bila kupata muda wa kupumzika